Matokeo ya leo Yanga SC yageuka shangwe Simba SC

Baada ya matokeo ya leo ya Yanga SC, Msemaji wa Klabu ya Simba SC, Haji Manara ameandika hivi katika Instagram yake, "Utopolo iliyobaki tupige embe mbichi tu,,,kutoka points nane now zimebaki mbili,"anaeleza.

Manara anamaanisha kuwa, muda wowote wanawafikia watani zao huko kileleni, ni baada ya Yanga ikiwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kugawana alama mojamoja na Namungo FC ya Lindi kwenye mchezo wa ligi raundi ya 11, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Aidha, Bigirimana Blaise, leo Novemba 22 amemwaga machozi baada ya dakika 90 kukamilika kutokana na kitendo cha kukosa penalti dakika ya 90 baada ya kipa namba moja wa Yanga kuiokoa kwa kuitema na aliporudia mara ya pili alipaisha mpira huo mazima.

Yanga ikiwa Uwanja wa Mkapa imelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Namungo kwenye mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho.

Mabao ya timu zote mbili yalipatikana kipindi cha kwanza ambapo Carlos Carlinhos alifunga bao la kwanza kwa Yanga dakika ya 13 kwa pasi ya Kibwana Shomari na dakika ya 16, Stephen Sey alipachika bao la kusawazisha kwa guu la kushoto.

Penalti ya Blaise iliyopaishwa ilipatikana dakika ya 90 baada ya beki,Bakari Mwamnyeto kumchezea faulo kiungo Shiza Kichuya ndani ya 18 na alionyeshwa kadi ya njano.

Mvutano mkubwa ilikuwa ni nani ambaye angepiga penalti hiyo jukumu likawa la Blaise mwenye mabao manne ambaye alikosa penalti hiyo baada ya Mnata kumsoma kwa umakini na kuipangua jumlajumla.

Sare hiyo inaifanya Yanga kugawana pointi mojamoja na Namungo FC Uwanja wa Mkapa huku Mnata akipewa zawadi ya noti na mashabiki baada ya kutimiza majukumu yake kwa umakini.

Yanga inafikisha jumla ya pointi 25 sawa na Azam FC ambayo ipo kileleni kwa idadi ya mabao huku Namungo ikibaki nafasi ya 9 na pointi zake ni 15.

Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, bao pekee la Hassan Materema dakika ya 63 limeipa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa kimeundwa na Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda/Ditram Nchimbi dk71, Feisal Salum, Michael Sarpong, Carlos Carlinhos na Farid Mussa/Deus Kaseke dakika ya 55.

Aidha kwa upande wa Namungo FC iliundwa na Jonathan Nahimana, Miza Chrstom/Haruna Shamte dk69, Edward Manyama, Hamisi Mgunya, Carlos Protas, Khamis Khalifa, Sixtus Sabilo/Iddi Kipagwile dk58, Freddy Tangalo, Steven Sey/Shiza Kichuya dk83, Lucas Kikoti na Bigirimana Blaise.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news