Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imetoa cheti cha pongezi kwa Diramakini Blog kwa kutambua mchango wake wa kutoa taarifa mbalimbali juu ya vitendo vya rushwa nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini (Dar es Salaam).
Diramakini blog ambayo inamilikiwa na Kampuni ya Diramakini Business Limited imekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa mbalimbali zinazohusiana na vitendo mbalimbali vya rushwa kutoka kila kona ya nchi.
Mbali na tukio hilo pia taasisi hiyo imezindua runinga ya mtandaoni inayofahamika kama TAKUKURU TV, hafla ambayo imefanyika leo Januari 28, 2021 katika ofisi za PCCB House Upanga jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Julius Mbungo katika hafla hiyo amesema kuwa, mchango wa vyombo vya habari nchini vimewezesha taasisi hiyo kufikisha taarifa kwa wakati kwa Watanzania juu ya namna ya kuzuia kuzuia kutoa na kupokea rushwa, hatua ambayo inawapa nguvu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutokomeza adui huyo kabisa hapa nchini.
"Sisi kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, tunatambua, tunathamini na tunawashukuru wanahabari wote na vyombo vyote vya habari kwa kuwa pamoja na sisi wakati wote wa mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini.
"Tuna uhakika kabisa kama siyo ninyi, juhudi hizi kubwa ambazo zinafanywa na Serikali yetu inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kupambana na rushwa, kutangaza uadui na rushwa isingeweza kufanikiwa kabisa.Hivyo, tunawashukuru kwa mchango wenu na endeleeni kutuunga mkono,"amesema Mkurugenzi Mkuu huyo.
Akizungumzia dhamira ya uzinduzi wa runinga mtandao ya TAKUKURU Tv, Brigedia Jenerali John Julius Mbungo amesema kuwa, lengo ni kuendelea kutoa elimu kwa umma ili uweze kufahamu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya jemedari Dkt.Magufuli katika kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo ni adui wa maendeleo.
"Ni kuufahamisha umma na Watanzania wote kwa ujumla juu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi wa mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli na ambaye ni jemedarai katika mapambano haya dhidi ya rushwa nchini, lakini pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kutokomeza rushwa, ufisadi,uonevu na dhuluma kwa wananchi wanyonge nchini.
Pia Brigedia Jenerali John Julius Mbungo amewataka wanahabari kutumia vema kalamu zao katika kuwaunganisha Watanzania, kuwa wamoja kuwashawishi kudumisha amani, kuchochea maendeleo na kuhamasisha kuendelea kupambana na maovu likiwemo janga kubwa la rushwa nchini.
Amesema, vyombo vyote vya habari vimekuwa mstari wa mbele kutoa elimu, hatua ambayo imewapa faraja kubwa katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kuzuia na kupambana na rushwa nchini.
Awali Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma kutoka TAKUKURU, Bw.Joseph Mwaiswelo amesema kuwa, tasisi hiyo inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wanahabari na vyombo vya habari nchini katika kutoa habari za kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ambazo zimewezesha kuyafikia matokeo chanya kwa nyakati tofauti.
"Tumewaita hapa leo kutokana na umuhimu wenu kwa TAKUKURU katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa. Tunatambua kwamba vyombo vya habari ni mdau muhimu na kiungo kikuu kati ya taasisi hii na jamii ya Watanzania ambayo ndiyo tunayoitumikia.
Bila kufikisha habari kwa wananchi kupitia Vyombo vya Habari, mambo kadhaa hayawezi yakafikiwa kwa mfano:Wananchi na wadau mbalimbali hawawezi kufahamu jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wengine kuzuia na kupambana na rushwa,
"Jamii haiwezi kufahamu rushwa ni nini na madhara yake kwa jamii ni yapi, hata ione umuhimu wa kuchukua hatua kuikabili, Mwananchi hawezi kufahamu haki zake na ni wapi afikishe malalamiko yake au taarifa kuhusu vitendo rushwa.
Hivyo, kama nilivyotangulia kusema, ninyi ndugu zetu katika tasnia ya habari ni wadau muhimu sana kwetu.
"Leo hii tumekutana hapa kwa ajili ya matukio muhimu mawili. Tukio la kwanza ni la kugawa vyeti kwa vyombo vya habari kwa kutambua mchango wenu katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa nchini. La pili, ni lile la kuzindua TAKUKURU TV, yaani chaneli ya televisheni mtandaoni ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
"Napenda kutumia fursa hii kueleza jukumu mojawapo la TAKUKURU kupitia Kurugenzi ya Elimu kwa Umma. Jukumu hilo la kisheria ni la kushirikisha umma katika mapambano dhidi ya rushwa kwa njia ya elimu. Jukumu hili na mengine yanatajwa katika Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007. Ili kutimiza matakwa hayo ya kisheria, tunafanya mambo mengi na hapa nitataja machache:
"Tunatumia klabu za wapinga rushwa shuleni na vyuoni kuwafikia na kuwaelimisha wanafunzi; tunaandaa programu za kuelimisha na kushirikisha vijana wasiokuwa katika mfumo rasmi wa elimu; tunaandaa semina au warsha kwa makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo watu wenye ulemavu (wa kusuikia na kutoona), wasanii, wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara;
"Tunaandaa na kurusha programu katika redio na televisheni mbalimbali hapa nchini ikiwemo kipindi maarufu cha redio kiitwacho ‘Rushwa Adui wa Haki’. Tunatumia machapisho mbalimbali kusambaza elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi kama vile magazeti, jarida la TAKUKURU, mabango, vipeperushi na brosha;Tunatoa elimu pia kupitia wavuti ya TAKUKURU na mitandao ya kijamii.
"Tunatekeleza haya yote huku tukizingatia matakwa ya Mkakati wa Mawasiliano wa TAKUKURU (PCCB COMMUNICATION STRATEGY) ambao pamoja na mambo mengine unahimiza juu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuelimisha na kuifikia jamii kwa wepesi na haraka zaidi.
"Ni kwa msingi huo, kuanzia mwaka 2019 tulianza kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii kama Instagram, Tweeter na Facebook na sasa tumeingia katika YOUTUBE kwa kuanzisha TAKUKURU TV. Juhudi zote hizi zinafanyika ili kuhakikisha tunamfikia mwananchi kadiri ya njia iliyo rahisi kwake kuitumia au kufikiwa na kumshirikisha katika mapambano dhidi ya rushwa,"amefafanua Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, Kampuni ya Diramakini Business Limited kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mwenza wa kampuni hiyo, James Nnko wameeleza kuwa, wamefarijika kwa namna ambavyo TAKUKURU kupitia uongozi mahiri wa Mkurugenzi Mkuu, Brigedia Jenerali John Julius Mbungo unavyotambua na kuthamini mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusiana na mambo mbalimbali yahusuyo njia za kuzuia na kupambana na rushwa nchini.
Nnko amesema kuwa, uwajibikaji wa makachero wa TAKUKURU chini ya Mkurugenzi Mkuu huyo umewezesha kurejesha matumaini na faraja kwa Watanzania wengi ambao kila siku jamii imeshuhudia namna ambavyo wamekuwa wakirejesha fedha za watu waliodhulumiwa kupitia mikopo umiza.
Amesema, kwa kazi hizo na nyingine nyingi ikiwemo kuiangazia na kuifuatilia miradi mbalimbali ya umma ambayo inatekelezwa katika nchi yetu, TAKUKURU imefanikiwa kuzuia vitendo vingi ambavyo vilikuwa na viashiria vya kudhoofisha maendeleo.
"Sisi Diramakini Business Limited kupitia blog yetu ya DIRAMAKINI tunatambua na tutaendelea kutambua kazi nzuri zinazofanywa na TAKUKURU kwa mustakabali wa maendeleo ya jamii zetu na Taifa letu, hivyo tunaomba Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Julius Mbungo apokee pongezi zetu hizi, nasi tunashukuru kwa kutambua umuhimu wetu kwao,"amesema Nnko.
Tags
Habari