NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Saa chache baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kutoa siku saba kwa Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga, Blasius Chatanda kuhakikisha vikundi vya uhalifu vinavyojiita watoto wa ibilisi vinamalizika katika Jiji la Tanga, kazi imeanza rasmi.
Taarifa za awali zilizoifikia DIRAMAKINI Blog zimebainisha kuwa, makachero maalum wameanza operesheni yao ambayo inaweza kupita mlango kwa mlango, hivyo wale wanaodhani vijana au watoto wao wanashiriki vitendo vya uhalifu ni vema wakatoa taarifa mapema kabla ya nyakua nyakua haijawafikia.
Hatua hii inakuja baada ya IGP Sirro kutoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kikao kilichoshirikisha wenyeviti wa serikali za mitaa, watendaji wa kata na madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Maagizo hayo ameyatoa ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea na kukagua hali ya ulinzi katika mikoa mbalimbali nchini.
Sirro ametoa agizo hilo kufuatia kuibuka kwa kundi la vijana wadogo wanaotembea kati ya 20 na kuendelea ambao hujihusisha na kufanya vitendo vya kihalifu huku wengine wakiwajeruhi baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali jijini hapa.
Kamanda Sirro amesema, Jeshi la Polisi limeweza kupambana na matukio makubwa katika Mkoa wa Tanga hivyo kikundi hicho kinachojiita watoto wa ibilisi hakitoweza kufanya vitendo vyovyote vya kihalifu kuanzia sasa, kwani jeshi hilo limejipanga kuwawajibisha.
“Kuhusu vikundi vya watoto wa Ibilisi maelekezo yangu kwa RPC nawapa wiki moja hiyo habari ya watoto wa ibilisi sitaki kusikia na kama watakuwepo katika huu mji nina uwezo wa kuingia ndani ya siku mbili tukamaliza.
"Hatuwezi kukaa na watoto wetu tena wadogo kisha tuwaite watoto wa ibilisi, viongozi wenzangu ipo haja ya kutazama malezi yetu, lakini pia kwa nini basi mnazaa watoto ambao hamuwezi kuwapa mahitaji yao kisha wanarudi kuwasumbua watanzania wenzao, hamuwezi kuwasomesha, kuwalisha na kuwatunza matokeo yake wanajiingiza kwenye uhalifu hii siyo sawa jamani wazazi wenzangu, “amesema.
Kamanda Sirro amewataka wazazi na walezi mkoani Tanga kuhakikisha watoto wao wasiwe kero kwa wengine kwani ni aibu kuona vijana wadogo wanatia dosari mji wa Tanga.
Tags
Habari