Na Rachel Balama, Diramakini Blog
TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mradi unaotumia teknolojia ya mionzi katika kuhifadhi vyakula visiharibike mapema ambapo itachochea uchumi wa viwanda na kuongeza pato kwa wakulima.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof.Lazaro Busagala wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya siku moja ya Kitaifa kwa Wahariri na Waandishi wa habari juu ya uelewa na udhibiti na matumizi salama ya mionzi nchini yaliyofanyika Juni 12,2021 mkoani Dar es Salaam.
Akifunga mafunzo hayo, amesema njia ya kuhifadhi mazao kwa teknolojia ya mionzi ni salama zaidi kuliko kuhifadhi kwa njia ya kemikali.
"Vyakula vinavyotunzwa kwa kutumia mionzi ni salama zaidi kuliko vile vinavyotunzwa kwa kutumia kemikali, mionzi inapokausha chakula haibaki kwenye chakula hicho," amesema Profesa Busagala.
Profesa Busagala ametoa mfano kwamba uhifadhi wa vitunguu kwa kutumia mionzi vinachukua miaka mitatu bila kuharibika ambapo kwa sasa kuna Mtafiti anaendelea kudadisi uhifadhi wa nyanya kwa kutumia teknolojia hiyo.
Amesema, mradi huo unatekelezwa na nchi 62 duniani na kwa Afrika nchi 6 ambapo Tanzania itakuwa nchi ya saba kutekeleza mradi huo kwa Afrika pindi utakapo kamilika.
Prof. Busagala ametaja mipango na matarajio mengine kuwa ni pamoja na kuanzisha mradi wenye kutumia teknolojia ya nyuklia katika kufanya tafiti mbalimbali zenye manufaa kwa nchi.
Amesema hiyo itaiwezesha Tanzania kuwa na viwanda vya madawa ya tiba za saratani pamoja na kutumika kama nyenzo ya kufundishia katika taasisi za elimu ya juu na tafiti.
Pia amesema kuwa wamejizatiti kuwa na mtambo wa kuzalisha vyanzo vya mionzi vinavyotumika kwenye matibabu, viwanda, kilimo na utafiti.
"Pia kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za matumizi salama ya mionzi ikiwemo ile ya uchimbaji salama na usafirishaji wa madini ya urani, kuwa na ofisi kila mkoa ili kuongeza uwezo wa kudhibiti matumizi ya teknolojia ya mionzi.
"Mipango mingine ni kuanzisha kituo cha mafunzo ya fani za Sayansi ya Nyuklia kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu pamoja na kuimarisha maabara ya TAEC ili iweze kutambulika kimataifa,"amesema.
Ametaja changamoto kubwa zinazoikabili TAEC kuwa ni watu wengi kutofahamu kazi na majukumu yake na wengi wanahisi ni mabomu kitu ambacho si sahihi.