Mwalimu Makuru amuangukia Rais Samia kuhusu tozo za miamala ya simu "HUU NI MTEGO KWA CCM"

Na Amos Lufungilo, Diramakini blog

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph anemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutumia hekima na busara zake kuwaokoa Watanzania wanyonge katika tozo kubwa za miamala ya simu.

Mwalimu Makuru ameyasema hayo katika mahojiano maalum na Mwandishi Diramakini mjini Musoma Mkoa wa Mara.

"Awali ya yote nichukue nafasi hii kumuomba sana...sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuangalia upya namna ambavyo Serikali yake itafanya ili kuwaokoa wanyonge hasa katika tozo za miamala ya simu.

"Kwani tozo hizo ambazo zilianza kukatwa kupitia miamala mbalimbali inayofanyika kupitia kampuni za simu tangu Julai 15, mwaka huu zimekuwa za kiwango cha juu sana.

"Ni tozo ambazo zinatoa maswali mengi baada ya kupendekezwa na Wizara ya Fedha na Mipango na hatimaye kupitishwa rasmi katika Bunge la bajeti ambalo limemalizika karibuni. Kwa haraka haraka, tozo hiyo imewaongezea mzigo wananchi katika gharama za uendeshaji wa maisha ya kila siku maana wananchi wanyonge hutegemea simu kufanya miamala katika shughuli zao za kila siku, kama vile biashara hivyo kutokana hali hivyo itasababisha faida kupungua katika biashara.

"Na inaweza kusababisha mzunguko wa fedha kupungua kwa wananchi, hivyo na kuleta mdororo wa kiuchumi kwa wananchi,pia wananchi wanyonge watapoteza ajira, kwani wengi walikuwa wamejiari kwa kufanya biashara hivyo inaweza kupunguza watumiaji kwa kuamia njia zingine,hii ni kutokana na makato makubwa ya kutoa na kutuma pesa,"amesema Mwalimu Makuru.

Mwalimu Makuru amesema, kwa sasa uchumi na maisha ya watu yamekuwa magumu maana hata biashara kwa miaka kadhaa imekuwa ngumu sana,hivyo Serikali haina budi kuangalia hili kwa kuwapunguzia tozo wananchi ili kuwapunguzia wananchi makali ya maisha.

Ameongeza kuwa, Serikali ina lengo zuri la wananchi kuchangia katika mfuko wa mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya wananchi katika nyanja mbalimbali kama vile miradi ya kimkakati ya kiuchumi,afya na elimu lakini, tozo walizoweka ni kubwa sana hivyo uwaumiza watanzania wanyonge.

Pia ameongeza kwa kusema wananchi wa vijijini watapata hadha kubwa sana kutokana na serikali kupandisha makato makubwa ya tozo,ambayo kimsingi itaongeza gharama za maisha ya wananchi wa vijijini.

Mwalimu Makuru ameongeza kuwa, kutokana na ongezeko la tozo za miamala ya simu zinaweza kuleta chuki kwa wananchi dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wanaongoza serikali,kwani vyama vya upinzani wanaweza kutumia kama ajenda kwa kupandikiza chuki kwa wananchi,"hivyo naomba Mwenyekiti wangu taifa wa Chama Cha Mapinduzi aweze kuingilia kati kwa kupunguza makato ya tozo za miamala ili iendane na hali ya maisha kwa sasa,"amesema.

"Huu ni mtego mkubwa sana kwetu, maana hata waliopitisha hizo tozo huko bungeni asilimia kubwa ni wabunge wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa mantiki hiyo, siku za usoni hatutakuwa na sehemu ya kujitetea maana jambo tumelifanya wenyewe na wanaoumia ni wananchi wetu ambao sisi ndiyo watetezi wao, hivyo tukirejea kwao, kuwaelezea kuhusiana na jambo lolote watakuwa wanatubeza, hii hali inahitaji busara na hekima ya juu,"amesema Mwalimu Makuru.

Pia alisisitiza kwamba, "naomba chama kuiangalia hii tozo kwa mapana, kwani hizo tozo ni kubwa sana, inatakiwa zipunguzwe angalau ziendane na hali ya maisha ya mtanzania mnyonge,ambapo CCM ndio chama pekee kinachotetea wanyonge hivyo hakuna budi Mwenyekiti au viongozi waweze kuliangalia kwa mapana kikiwa kama chama tawala.

"Naombeni kuwakumbusha watanzania wenzangu kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano ilisitisha sheria ya kikokoto cha wafanyakazi maana ilikuwa ni kandamizi kwa wafanyakazi wanyonge, ambayo ingewadhulumu sana watumishi wastaafu.

"Hivyo hata katika hili la tozo za miamala namuomba Mwenyekiti alitazame kwa makini, kwani halina utofauti na kikokoto maana makato ya tozo ni kubwa ni kama uunyang'anyi na uporaji wa pesa za wananchi wanyonge,"amefafanua Mwalimu Makuru.

Ameongeza kuwa,anaomba kampuni za simu zipunguze gharama kusudi watanzania wanyonge waweze kunufaika na uwepo wa hizo kampuni kuliko kujali faida tu. "Maana kuna baadhi ya makampuni wana gharama nafuu kuliko mengine katika kufanya miamala mfano Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),"amesema.

Mwalimu Makuru alibainisha kuwa,viongozi wa chama katika ngazi zote za chama wanapaswa kushikamana kukemea maovu pasipo kufumbia macho, "ila na mazuri yanayofanywa na serikali tuyaseme kwa wananchi kwa maslahi mapana ya taifa,"amesema.

"CCM imara,Tanzania imara,chama legelege uzaa Serikali legelege,ninaamini Chama Cha Mapinduzi kipo imara kwa kuwatetea wanyonge na kuwaletea wananchi maendeleo.Mungu ibariki Tanzania,"ameongeza.

Rai hiyo inakuja baada ya Julai 15, 2021 kampuni mbalimbali kuanza kutekeleza agizo la Serikali la kutoza tozo kwa miamala mbalimbali ambayo imekuwa ikifanyika kupitia simu iwe kwa kutuma au kutoa.

Aidha, utekelezaji wa mfumo huo mpya ambao umezua mjadala mkali nchini, ulianza ikiwa ni siku mbili tu, baada ya kampuni za simu za mikononi kuanza kuwatumia ujumbe mfupi wateja kuwajulisha kuhusiana na kuanza rasmi kutekeleza kwa ukataji wa tozo hizo.

Kodi ya uzalendo ambayo inaanzia shilingi 10 hadi shilingi 10,000 kulingana na ukubwa wa muamala, wananchi wanaitaja kama mzigo mkubwa katika maisha yao ya kila siku.

Mfano kabla ya kodi ya uzalendo, wateja wa Airtel Money walikuwa wanakatwa shilingi 350 tu ndani ya mtandao kutuma shilingi 15,000 lakini sasa wanalipa shilingi 960 na walikuwa wanakatwa shilingi 550 kwenda mtandao mwingine, lakini imepanda mpaka shilingi 1,160.

Aidha,watakapotaka kutoa fedha hizo watalipia shilingi 2,010 badala ya shilingi 1,400 ya mwanzo. Hii inamaanisha ndani ya mualama wa shilingi 15,000 kutokana na gharama pamoja na tozo, mteja atalazimika kukatwa kiasi kikubwa zaidi.

Pia kwa wateja wa Mpesa, kutuma shilingi 15,000 kwenda kwa mteja asiyesajiliwa, makato ni shilingi 970 kutoka shilingi 360 wakati ikigharimu mtu shilingi 2,820 kwa mteja asiyesajiliwa kutoka shilingi 2,210 ambayo inajumuisha na tozo ya Serikali.

Wakati huo huo, kwenda mitandao mingine, kiasi hicho kitalipiwa shilingi 1,160 kutoka shilingi 550 iliyokuwapo na watakaopelekwa kwenye akaunti zao za benki watakatwa shilingi 1,810 badala ya shilingi 1,200 iliyokuwapo. Kutoa kiasi hicho iwe kwa wakala au ATM wanakatwa shilingi 2,060 kutoka shilingi 1,450. Vivyo hivyo katika mitandao mingine ikiwemo Halotel, Tigo Pesa na nyinginezo.

Ukiangalia ukokotoaji wa tozo hizo utaona kuwa, mtu aliyekuwa akipokea fedha kiasi cha shilingi 100,000 kutoka kwa wakala alikuwa akikatwa shilingi 3,600 sasa atakuwa akikatwa jumla ya shilingi 6,100 na kiwango hicho kinazidi kupanda kadri muamala wa fedha unavyoongezeka.

Hivi karibuni wakati akizungumza kwenye kipindi cha 360 cha kituo cha Clouds TV, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema, hiyo sio tu ni kodi, "bali tunatunisha mfuko wa mshikamano. Tutachangia kupitia makato ya simu,”alisema, huku akiongeza kuwa,

"Itakuwa ni aibu kwa miradi ya maendeleo kukwama kwa kuwa Serikali imeshindwa kukusanya kodi.Kuna mambo hayapaswi kuwepo. Haitakiwi kuona kijiji hakina barabara inayopitika muda wote na tunabeba wagonjwa juujuu. Mbona tunaweza miito ya simu na kukatwa hela nyingi tu kwa nini isiwe kutunisha mfuko wa mshikamano?," amesema na kuhoji Waziri Dkt.Nchemba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news