NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa wa Kanisa la Penuel Healing Ministry la Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam, Alphonce Temba amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuangalia namna ya kusaidia ili wanachama wa iliyokuwa kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) waweze kulipwa fedha zao.
Wito huo ameutoa jijini Lusaka nchini Zambia ambapo yupo kwa mwaliko maalum kushiriki hafla ya kumuapisha Rais mteule wa nchi hiyo, Mheshimiwa Hakainde Hichilema anayetarajia kuapishwa kesho.
Mwaliko huo umekuja baada ya utabiri wake kuhusu ushindi wa Chama cha Upinzani cha United Party for National Development (UPND) kutimia kwa asilimia zote.Unaweza kusoma kuhusu utabiri wa Mwinjilisti Temba nchini Zambia hapa>>>
Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya Video Coference (Zoom) nchini Tanzania muda mfupi baada ya kupokelewa na mwenyeji ambaye ni Mwenyekiti wa chama kilichoshinda uchaguzi nchini Zambia, Stephen Katuka, Mwinjilisti Temba amesema, Watanzania wana imani kubwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutokana na moyo wake wa huruma, usikivu na upendo kwa wote.
"Mheshimiwa Rais, kwa huruma yako, naomba Serikali yako iliangalie suala la DECI kwa mtazamo wa rehema na huruma.
"Mungu amekuwa akinionyesha na kunisisitiza nizungumzie jambo hili,niweze kukumbushia kuwa, wakati DECI ilipofika kwetu (Watanzania) ilijitambulisha kama kampuni iliyosajiliwa kihalali BRELA na ilikuwa inalipa kodi kama kampuni nyingine,kitendo ambacho kiliwavutia wananchi wanyonge, maskini wa nchi hii kujiunga.
"Hakukuwa na udangayifu wowote uliowahi kujitokeza kati ya DECI na wanachama wake, watu walilipwa hela zao kwa wakati, kila walipofikia tarehe za malipo, hadi pale Serikali ya Awamu ya Nne iliposimamisha shughuli za kampuni hiyo.
"Mwaka 2009, kwa ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu mstaafu kwa sasa, Mizengo Kayanza Peter Pinda kwamba fedha zetu zipo salama na zitarajeshwa kwa wananchi na wala Serikali ya CCM haitawadhulumu wananchi wake. Hilo lilitupa matumaini makubwa kwa Serikali yetu ya CCM.
"Isitoshe Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam baada ya kusikiliza shauri lililofunguliwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali dhidi ya wakurugenzi wa DECI mahakama hiyo iliamuru kuwa, fedha za wanachama waliokuwa wamepanda mbegu zao DECI zirejeshwe kwa wananchi hao.
"Lakini ofisi ya DPP iliendelea kung'ang'ania fedha hizo kwa kukata rufaa Mahakama Kuu ikidai kuwa, fedha hizo zitaifishwe na Serikali.
"Jambo ambalo Mahakama Kuu ilikataa na ikakubaliana zirejeshwe mikononi mwa wananchi zaidi ya laki sita ambao hawajawahi kushtakiwa na kupatikana na hatia.
"Kutokana na mvutano unaoendelea mahakamani mpaka sasa tunamuomba Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake sikivu ya CCM ituonee huruma sisi wananchi wanyonge na maskini tuweze kurejeshewa fedha zetu ambazo tumeteseka kuzipata hadi sasa,"amefafanua kwa kina Mwinjilisti Temba akiwa hapa jijini Lusaka.
Amesema, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imempa mamlaka kisheria Rais kutoa nafuu ya maelekezo kwa ajili ya haki.
MUHIMU
UNATAMANI DIRAMAKINI BLOG TUWE HEWANI SAA 24 KUKUPA HABARI ZA KINA KILA DAKIKA, TUNAOMBA UTUUNGE MKONO KWA KUCHANGIA GHARAMA ZA MAWASILIANO NA INTANETI KWA WAANDISHI WETU POPOTE WALIPO NDANI NA NJE YA TANZANIA; TUNAPOKEA MCHANGO WAKO KUPITIA 0719254464 (Tigo Pesa-Godfrey Nnko) AU UKIHITAJI NAMBA YA BENKI TUJULISHE. MUNGU AKUBARIKI SANA KWA SAPOTI YAKO. ASANTE