DCEA: Tuleteeni taarifa zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema kuwa, kila Mtanzania ana wajibu wa kutoa taarifa yoyote inayohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya hapa nchini.

"Mamlaka tunafanya kazi kutokana na jamii. Kwa niaba ya Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Gerald Kusaya niwahakikishie kuwa, mtu au watu ambao wataleta taarifa zao katika mamlaka zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya, tutazipokea kwa uaminifu wa hali ya juu na tutamtunzia siri, hivyo msiwe na hofu yoyote kama mna taarifa.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA akielezea kuhusiana na mamlaka hiyo katika mkutano na waandishi wa habari za kidijitali kinachofanyika mkoani Morogoro. (Na Mpigapicha Wetu).

"Nirejee wito huu kwamba, endeleeni kutuma au kuleta moja kwa moja taarifa zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya, zitapokelewa kwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi;

Hayo yamesemwa leo Novemba 10, 2021 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Florence Khambi wakati akielezea kuhusiana na mamlaka hiyo katika siku ya kwanza ya kikao kazi cha waandishi wa habari za kidigitali kinachofanyika katika Ukumbi wa Queen Hotel iliyopo mkoani Morogoro.

Mkuu huyo amebainisha kuwa, dawa za kulevya ambazo ni tatizo kubwa hapa nchini ni pamoja na bangi na mirungi.

Kwa sheria ya Tanzania, mtu ukifanya kilimo cha dawa za kulevya mfano ukilima bangi na mirungi (dawa za mashambani) au ukikutwa na mbegu zake, ukikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30 na kosa hili halina dhamana.

Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 ambayo ilianza kutumika kuanzia Mwezi Septemba 2015 na kurejewa mwaka 2019.
Wakati huo huo, Khambi amesema kuwa, dira yao kama mamlaka ni kujenga jamii ya Tanzania isiyotumia dawa za kulevya au kushiriki katika biashara ya dawa hizo na hivyo kuchangia lengo kuu la kuwa na maisha bora nchini kama ilivyochagizwa kwenye malengo ya maendeleo ya 2025.

"Na dhima yetu ni kujenga mfumo bora wa kudhibiti na kupambana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya na kuendeleza ushirikiano katika hatua mbalimbali za udhibiti wa dawa za kulevya na kujenga uwezo wa taasisi na asasi zisizo za kiserikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya,"amefafanua.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Florence Khambi amesema, majukumu ya mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazoelekezwa katika udhibiti wa dawa za kulevya.

"Hivyo, katika kutekeleza majukumu hayo mamlaka inafanya kazi ya kusimamia utekelezaji wa mikataba ya Kimataifa, maazimio na makubaliano katika kudhibiti dawa za kulevya, kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti dawa za kulevya,"amesema.

Khambi amesema kazi nyingine ni kutengeneza miongozo inayoelezea tatizo la dawa za kulevya na madhara yake katika jamii.

"Pia kuboresha na kurekebisha sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya,kuhamasisha udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kusambaza taarifa kwa umma na juhudi nyingine za udhibiti.

Na kazi nyingine ni kuchukua hatua stahiki za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zikiwemo kukamata, kupekua na uchunguzi wa masuala yanayohusiana na dawa za kulevya.

"Pia kuzuia, kupeleleza na kuchunguza uchepushaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya pamoja na kemikali zilizosajiliwa kutoka kwenye vyanzo halali wakati huo huo kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa matumizi ya tiba, biashara na mahitaji ya kisayansi na kuanzisha mfumo thabiti wa ukusanyaji taarifa na uchambuzi katika ngazi ya taifa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya,"amesema.
Khambi ameendelea kufafanua kuwa, kazi nyingine ya DCEA ni kuhamasisha, kuratibu na kuhakikisha jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti wa dawa za kulevya zinaimarishwa na kufanya, kuwezesha na kuratibu tafiti zinazohusiana na dawa za kulevya.

"Mamlaka pia inajishughulisha na kazi ya kuratibu na kuwezesha wadau wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

"Kutoa mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, fedha haramu na kemikali bashirifu na kufanya uchunguzi wa sayansi jinai,"amefafanua Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Florence Khambi wakati akielezea kuhusiana na DCEA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news