DCEA yasisitiza uvutaji wa shisha ni kirusi hatari, Dkt.Mlondo afichua yaliyofichika

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema ongezeko la wimbi la watumiaji wa shisha umesababisha madhara makubwa kwa jamii na hata kuhatarisha afya zao.

Ni baada ya baadhi watumiaji kuanza kutumia kifaa hicho ambacho ni utamaduni wa wenzetu huko nje wanaokitumia kwa matumizi ya tumbaku kuchanganyia dawa haramu za kulevya.
Kamishina Msaidizi wa Kinga na Huduma kwa Jamii wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Moza Makumbuli ameyabainisha hayo leo Novemba 10, 2021 wakati akiwasilisha mada kuhusu dawa za kulevya na madhara yake.

Ni katika siku ya kwanza ya kikao kazi cha waandishi wa habari za kidigitali ambacho kimefanyika katika Ukumbi wa Queen Hotel mkoani Morogoro.

Makumbuli amesema kuwa, kitendo cha mtu kuvuta shisha kwa saa moja ni sawa na mtu kuvuta sigara kati ya 100 hadi 200 jambo ambalo ni hatari zaidi kiafya.

Amesema, hali hiyo imekuwa ikichochewa na watu wenye nia mbaya ambao huwa wanaongeza madawa ya kulevya katika mchanganyiko huo ili kupata kilevi.

Amesema kuwa, uhalifu wa dawa za kulevya upo mitaani na kila mmoja atambue kuwa, shisha ni utamaduni ambao umekuja hapa nchini kutoka nje na haupaswi kupewa nafasi katika jamii zetu.

"Na imekuwa ikitumika tofauti na wenye utamaduni wao, ambao kiuhalisia kifaa hicho walikuwa wanakitumia kuvutia tumbaku, lakini sisi zinaongezwa ladha mbalimbali na wakati mwingine kuwekwa dawa za kulevya,"amesema.

Katika kuhakikisha, mamlaka hiyo inachukua hatua za haraka kudhibiti matumizi ya shisha na aina zingine za dawa za kulevya, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kuzuia Dawa za Kulevya, Florence Khambi amesema,wanalifanyia kazi na taarifa zaidi watakuwa wanatoa ili kuhakikisha Taifa linakuwa salama bila dawa za kulevya.
Wakati huo huo, Kamishna Msaidizi Moza Makumbuli amesema, kwa sasa tatizo kubwa linaloikumba jamii ni kukithiri kwa matumizi ya dawa zilizochepushwa kutoka katika matumizi halali na kugeuzwa dawa za kulevya kwa waraibu wa dawa hizo.

Makumbuli amezitaja dawa tiba hizo zenye asili ya kulevya ni Pethidine, Morphine, Ketamine, Fentanyl, Tramadol, Phenobarbitone, Codeine, Hydrocodone, Oxycodone, Methylphenidate (Ritalin), Benzodiazepine (Valium) Dextromethorphan (DXM) na Loperamide.

DAKTARI MLONDO

Daktari Kalegamye Hinyuye Mlondo ameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, watumiaji wa shisha wanapaswa kutambua kuwa ina madhara mengi na hatari kwa afya ya binadamu

Shisha ni nini?

Dkt.Mlondo anasema, shisha ni tumbaku iliyochanganywa na ladha za harufu ya kuvutia kama matunda aina mbalimbali ikiwemo vannila au chocolate.

"Shisha inapatikana sana maeneo ya starehe nje na ndani ya nchi na imejizolea umaarufu mkubwa sana hasa kwa vijana, bahati mbaya kuna vijana wengi hutumia shisha, lakini hawavuti sigara huku wakidhani shisha ni kitu kingine kabisa tofauti na sigara.
"Lakini leo napenda kuwaambia shisha ni zaidi ya sigara na madhara yake ni makubwa zaidi ya yale ya sigara.Hivi karibuni Serikali ya Tanzania imepiga marufuku matumizi ya shisha, lakini ikapingwa na vijana wengi ambao wengi wao huvuta kwa kuiga na kutaka kuonekana wa kisasa bila kujua madhara yake kiafya, hivyo ni vema wakatambua kuwa, shisha ina madhara mengi,"amesema Dkt.Mlondo.

Dkt.Mlondo anasema, miongoni mwa madhara yatokanayo na shisha ni pamoja na saratani za aina mbalimbali.

"Shisha inavutwa tofauti kidogo na sigara,yaani inavutwa mara nyingi kwa muda mfupi, huvutwa ndani zaidi ya mapafu na kwa kutumika muda mrefu yaani zaidi ya saa moja tofauti na sigara ambayo inavutwa dakika tano na kuisha.

"Lakini pia tofauti na sigara ambayo inasababisha saratani ya mapafu tu mara nyingi shisha inaleta saratani mbalimbali ikiwemo za figo, koo, mapafu, kibofu cha mkojo, ubongo na damu kwa wakati mmoja.Shisha ina mchanganyiko wa kemikali nzito ambazo kitaalamu zimethibitika kusababisha saratani, utafiti unaonyesha kuvuta shisha kwa saa moja ni sawasawa na kutumia sigara 100 mpaka 200,"anafafanua Dkt.Mlondo.

Pia Dkt.Mlondo anasema kuwa, shisha huwa inasababisha uraibu au mazoea kwani ina tumbaku kama sigara za kawaida.

"Ina kemikali inayoitwa kitaalamu kama nicotine ambayo mwili ukiizoea basi unaitaka mara kwa mara, ukizoea shisha hutaweza kuacha kirahisi na hata siku ukisafiri sehemu ambayo haipo basi utalazimika kuvuta sigara ili kukidhi haja ya mwili, hivyo mvuta shisha ataishia kuwa mvuta sigara, jambo ambalo ni hatari kiafya,"amebainisha.

Daktari huyo anaendelea kufafanua kuwa, pia matumizi ya shisha huwa yanasababisha kusambaza magonjwa kwani mara nyingi shisha inatumika na watu zaidi ya mmoja, wakati mwingine hata wasiofahamiana.

"Kama ule mpira usipooshwa vizuri, basi magonjwa kama kifua kikuu na pneumonia ya fangasi huweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine, lakini hata ikioshwa vizuri basi kuchangia na mgonjwa wakati huo huo huweza kuleta maambukizi ya bacteria wa madonda ya tumbo kitaalamu kama helocobactor pylori huweza kuambukizwa pia.

"Vilevile uvutaji wa shisha una madhara kwa mtoto aliyepo tumboni, hii ninamaanisha kuwa, mama mjamzito kama ilivyo kwenye uvutaji wa sigara husababisha madhara makubwa kwa mtoto, ikiwemo kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo sana au kuzaa mtoto asiye na baadhi ya viungo kama mikono au miguu, kitalaamu tunaita tetatorogenic effect,"anabainisha Dkt.Mlondo.

Mbali na hayo, Dkt.Mlondo anasema, shisha ni hatari kiafya kwani huwa inachangia kwa kiwango kikubwa magonjwa ya kinywa.

Anasema, mkusanyiko wa kemikali ya nicotine kwenye damu na mate mdomoni husababisha magonjwa ya meno na fizi ambayo huharibu sana meno na kumfanya mtu abaki bila meno ya kutosha.

"Lakini pia huwa inasababisha magonjwa ya moyo, kwani shisha huharibu mishipa ya damu na kuifanya iwe membamba sana kupitisha damu, hivyo husababisha shinikizo la damu kupanda na shambulio la moyo kitaalamu kama heart attack.

"Sambamba na kuharibika kwa ubongo, kwani kemikali ya nicotine na compound zingine zinazopatikana kwenye shisha huweza kuzuia damu kufika vizuri kwenye ubongo, hali hii husababisha kiharusi, ugonjwa ambao huanza na dalili za kushindwa kuongea na kupoteza nguvu za nusu ya mwili wa binadamu,"amefafanua Mtaalamu huyo wa afya.

Dkt. Mlondo ameendelea kufafanua kuwa, matumizi ya shisha huwa yanamaliza nguvu za kiume, kwani kemikali za kwenye shisha pia huweza kuziba damu ambayo inaenda kwenye sehemu za siri.

"Hii huua nguvu za kiume kabisa kwa watumiaji wanaume, vivyo hivyo, huwa inasababisha ugumba kwani mirija inayopitisha mayai ya mwanamke kitaalamu kama fallopian tubes huzibwa na kemikali ya nicotine na kusababisha mbegu za mwanaume kushindwa kulifikia yai la mwanamke.

"Pia huleta makunyazi ya ngozi, kwani mkusanyiko mkubwa wa kemikali ya nicotine kwenye ngozi, mate, damu na kila aina ya maji ya mwili humfanya mtumiaji aonekane mzee kuliko umri wake halisi kitu ambacho watu wengi hawakipendelei,"anasema Dkt. Mlondo.

Mtaalamu huyo wa afya anabainisha kuwa, yapo madhara mengi ya kiafya lakini, aliyoyabainisha ni baadhi tu ya madhara ambayo yamegundulika mpaka sasa na huenda kuna mengine ambayo watafiti bado hawajayagundua.

"Nichukue nafasi hii kutoa rai kwa vijana na Watanzania kwa ujumla, wasivute shisha kufurahisha marafiki, vivyo hivyo usivute kwa sababu umelewa, usivute kwa sababu unataka kuonekana mjanja na usivute kwa sababu una msongo wa mawazo.

"Ndugu yangu kumbuka kila mvutaji ana kinga ya mwili tofauti na mwenzake na kila mtu ataingia kwenye jeneza lake mwenyewe, lakini pia taifa haliko tayari kupoteza nguvu kazi ya vijana, vijana amkeni mfanye kazi, achaneni na mambo ambayo hayana tija katika maisha yenu, kwani matumizi ya madawa ya kulevya ni hatari kwa afya yako,"amesisitiza Dkt. Mlondo.

UFANYE NINI ILI KUJINASUA?

Kamishina Msaidizi wa Kinga na Huduma kwa Jamii wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Moza Makumbuli anasema kuwa, kuna namna nyingi ambazo unaweza kujinasua katika matumizi ya dawa za kulevya.
"Mosi ni kujitambua kuepuka makundi hatarishi, kuepuka tamaa, kutoa taarifa kwa wakati kuhusiana na watu au kikundi cha watu ambacho kinajihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kuepuka unyanyapaa kwa waraibu wa dawa za kulevya, badala yake tuwe nao karibu na kuwapa elimu kuhusiana na athari za matumizi hayo,"amesema Makumbuli.

Pia amesema kuwa, DCEA imeendelea kuwajengea uwezo wadau mbalimbali ambao wataendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na madhara mbalimbali ya matumizi au kujihusisha na dawa za kulevya wakiwemo wanahabari ili kutumia kalamu zao kufikisha ujumbe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news