NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Tanzania imeendelea kuziendea fursa mbalimbali duniani ambazo zinaipa mwanga Sekta ya Utalii kwa ajili ya kuvutia watalii kutoka kila kona ya Dunia ili kuja nchini kutembelea vivutio vilivyopo.
Kwa mujibu wa tovuti Kuu ya Serikali, Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zilizojaaliwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya utalii kuanzia maeneo ya kihistoria (Mapango ya Amboni na mengineyo, Hifadhi ya wanyama ya pori ya Gombe katika mkoa wa Kigoma yenye Sokwe, miji ya Bagamoyo, Kilwa na Zanzibar- mji Mkongwe na nchi ya marashi na viungo).
Hifadhi za Taifa zikiwemo Manyara, Serengeti, Mikumi, Seleous, Ngorongoro na hifadhi nyingi za wanyama zenye wanyama na ndege wa aina mbalimbali.
Milima iliyopo kama vile mlima Meru na mlima wenye volkano wa Oldonyo Lengai na mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu sana barani Afrika, Kreta ya Ngorongoro na Bonde la Olduvai linalosemekana kuwa ni chimbuko la binadamu wa kwanza.
Tanzania iko katika eneo zuri la kijiografia lenye mwambao mrefu wa pwani kwa ajili ya biashara ya kimataifa (zikiwemo fukwe mpya zinazojitokeza) kwa kuwa inahudumia nchi sita za bara zisizo na bandari.
Aidha, imezungukwa na maziwa makuu ya Tanganyika, lenye kina kirefu zaidi barani Afrika, Ziwa Victoria ambalo ni miongoni mwa maziwa makubwa duniani- lenye wingi wa samaki wa maji baridi na Ziwa Nyasa lililopakana na Malawi.
Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa haraka sana nchini Tanzania na kuongoza kwa kuchangia pato la Taifa (GDP) na pia ni miongoni mwa sekta zinazoongoza katika kuliingizia taifa fedha za kigeni.
Royal Tour
Kwa kutambua mchango mkubwa unaotokana na Sekta ya Utalii nchini, hivi karibu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alirekodi makala ya kutangaza vivutio vya utalii, biashara na uwekezaji.
Makala ambayo itaoneshwa hivi karibuni kwenye kipindi maarufu cha Royal Tour, juhudi hizo ndizo zinawafanya wasaidizi wake kila mmoja kuhakikisha kupitia sekta ya utalii anaongeza ubunifu ilii kuipaisha zaidi sekta hiyo ambayo inatajwa kuwa na matokeo ya haraka kwa mataifa mbalimbali duniani.
Maonesho ya FITUR
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi -Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Pascal Shelutete amesema, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki Maonesho ya Utalii nchini Hispania yanayofahamika kama FITUR kuanzia tarehe 19 hadi 23 Januari, 2022.
Shelutete amesema, Maonesho ya Fitur yanayofanyika katika Jiji la Madrid na ni mojawapo ya maonesho makubwa ya utalii duniani na Hispania ni nchi ya 11 kwa kuleta watalii wengi nchini Tanzania.
"Maonesho haya yanafanyika kwa mara ya kwanza kwa kukutanisha nchi mbalimbali baada ya kutofanyika mwaka jana 2021 kutokana na janga la UVIKO-19,"ameeleza Shelutete.
FITUR ni nini?
Haya ni maonesho ya siku tano, zenye shughuli nyingi katika maonesho na makongamano ya biashara kimataifa katika sekta ya utalii. Ni siku ambazo kulingana na vivutio vya utalii viliyopo hapa Tanzania zinatoa ishara njema ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kuutangaza utalii wetu Kimataifa.
Ushiriki wa Tanzania katika siku hizi tano ambazo hutafsiri kuwa na mamia ya fursa za kufanya mawasiliano, kuanzisha miradi na kufanya makubaliano pia unawawezesha kufikia wadau wengi kwa wakati mmoja.
Miongoni mwao ni wataalamu walio na kiwango cha juu cha uwezo wa kufanya maamuzi katika sehemu yoyote ya utalii, wenyeviti,mameneja wakuu,wasimamizi wa masoko,mauzo,biashara na wasimamizi wa mauzo na washauri katika sekta ya utalii.
Kupitia FITUR pia, Tanzania kupitia Sekta ya Utalii inajumuika na makundi mbalimbali ya watu ambao utalii ni sehemu ya maisha yao ya kila siku, hivyo kuongeza mawazo mapya na vyanzo vya biashara.
Pia ushiriki wa Tanzania, ni moja wapo ya hatua muhimu kwani maonesho hayo yanaweza kuwatangaza zaidi ikizingatiwa kuwa, kwa mujibu wa waratibu wa maonesho hayo kuna zaidi ya vyombo vya habari 1,170 kutoka kila kona ya Dunia, hivyo ni njia muhimu katika kujitangaza zaidi.
Kwa nini ushiriki wa Tanzania kwenye FITUR?
Mosi ni njia rahisi ya kufanya mawasiliano mapya na kupanua mtandao wa sekta ya utalii nchini, pili ni kuongeza fursa za biashara na tatu ni kukutana na wauzaji wapya na wateja na kuimarisha uhusiano uliopo wa biashara.
Maonesho haya ya Utalii yanatajwa kuwa moja ya eneo muhimu zaidi la kukutania kimataifa kwa wataalamu na vinara wa masoko kupitia Sekta ya Utalii na yamekuwa yakiwaunganisha pamoja wadau mbalimbali kutoka mataifa mengi yakiwemo ya Amerika Kusini.
Kwa mwaka 2018, makampuni zaidi ya 10,000 yalishiriki katika tukio hilo kubwa, ambalo hutumikia kwa maonesho ya sekta hii.
Ni jukwaa ambalo linaongoza kwa masoko ya ndani na nje. Washiriki wengi kutoka mataifa tofauti tofauti wamekuwa wakineemeka kupitia maonesho hayo kwa kujitangaza, kuwasilisha bidhaa mpya,kujifunza kuhusu mbinu mbalimbali za kuvutia watalii kulingana na vyanzo vyao, kubadilishana mawasiliano na washiriki mbalimbali ambao uhamasishana kwa ajili ya kufanya utalii katika maeneo wanayovutiwa nayo.