NA DIRAMAKINI
WADAU wa Uhifadhi, Rasilimali na Watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wamesema, endapo juhudi za haraka hazitachukuliwa na Serikali juu ya uwepo wa shughuli za binadamu ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro upekee wa hifadhi hiyo utapotea.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, Mratibu wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (Media Center for Resources Advocacy), Habib Mchange amesema, hali ndani ya hifadhi hiyo inatisha.
Amesema,Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ipo hatarini kupotea na kupoteza uhai na umashuhuri wake kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo ufugaji uliopitiliza, ujenzi wa nyumba zisizofuata taratibu za kihifadhi na shughuli nyingine za kibiashara.
‘’Nimeshuhudia mambo ya hovyo yakifanyika na sisi kama wanaharakati hatupendi na haturidhishwi na kupotea kwa asili hiyo, ambapo nimeona mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda, kuku, na mingineyo ikichukua eneo kubwa kuliko wanyama wa asili wanaopendwa kufuatiliwa na watalii,’’ amesema.
Kwa mujibu wa Mchange, pamoja na kuzingatia ukweli kuwa Ngorongoro ni hifadhi na eneo la kipekee linalohusisha wanyama, binadamu na mifugo kwa pamoja, lakini hali ilivyo kwa sasa inatisha kiasi cha kutishia usalama wa hifadhi na wananchi husika wa asili wanaoishi katika eneo hilo.
Amesema, mwaka 1959 wakati wakazi walioruhusiwa kuishi katika hifadhi hiyo kwa mchanganyiko wao na wanyamapori, wakazi hao hawakuzidi watu elfu tisa tofauti na sasa wakazi hao wamefika zaidi ya laki moja na mifugo yao wanayoimiliki ikikadiriwa kuwa zaidi ya laki sita.
‘’Nimefanya nao mahojiano wanasema kuna mifugo laki mbili na nusu, sio kweli na ningewaomba sana waandishi wa habari, hii ni ajenda ya taifa na tunapaswa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kulifanya eneo hilo kuwa bora na lidumu zaidi kuliko sasa kuwepo na shughuli nyingi za binadamu,’’ amesema.
Kwa upande wake, mtalii kutoka nchini Ujerumani, Paul Schenzern amesema, hali inatisha na inaondoa ile ladha au uzuri waliokuwa wanauona kipindi cha nyuma, hivyo mamlaka husika zifanye jitihada za kuwaondoa watu na kulifanya eneo hilo kuwa nzuri na la kipekee kama ilivyokuwa awali.
Amesema, kuna siku alifanya utalii katika eneo hilo, ambapo kwa muda wa saa tatu akiwa ndani ya hifadhi hiyo alikuwa anakutana na makundi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo huku wanyama wengine waliokuwepo wakiwa hawaonekani sana.
Schezern amesema anaifahamu Ngorongoro kwa kuwa ina eneo bora zaidi la kiutalii na kamwe hakuwaza kama angepita barabani anapishana na mifugo kama ng’ombe japokuwa alikuwa anafahamu kuwa Ngorongoro wanaishi binadamu na wanyama, lakini si kwa kiwango alichokiona sasa.
‘’Nimetembea hifadhi kadhaa duniani ambazo wanyama na binadamu wanaishi kwa asili, kwa kweli zinavutia na hata kuishi kwao kunaendana na uhifadhi wa mazingira, tofauti na hapa Ngorongoro na unapata shida kuwashawishi watu kuendelea kwenda Ngorongoro,"amesema.
Hivyo, amesema kuna ulazima wa mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kuchukua hatua stahiki ikiwemo kumuunga mkono Rais Samia juu ya uhifadhi endelevu katika eneo hilo muhimu kwa watalii duniani.
Tags
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro
Habari
Maliasili na Utalii
Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania