NA GODFREY NNKO
SERIKALI imesema kuwa, Sekta ya Madini nchini imeendelea kukua kwa kasi, hivyo kuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.
Imeelezwa hadi sasa Sekta ya Madini imechangia asilimia 7.9 ya pato la taifa.
Hayo yamesemwa leo Februari 23, 2022 na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa wakati akifunga Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania kwa mwaka 2022.
Mkutano uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere kilichopo jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 22 hadi leo.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema wizara hiyo itaendelea na usimamizi na uratibu wa shughuli zote za uchimbaji wa madini pamoja na kushirikiana na wadau ili kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha Watanzania.
Akitoa salamu kwa uwakilishi wa mawaziri waalikwa kutoka Nje ya Nchi, Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi, Mheshimiwa Ibrahimu Uwizeye amesema, Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika sekta ya madini.
Pia amesema, Tanzania imekuwa darasa kubwa kwa nchi jirani kutokana na mafanikio makubwa yaliyotokana na uchimbaji wa sekta ya madini.
Akihutubia katika mkutano huo, Waziri Mkuu amesema, mchango huo umetokana na jitihada zilizofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa madini.
Sambamba na ushirikiano baina ya wadau pamoja na sera nzuri na mazingira rafiki yaliyowekwa na Serikali kwa wawekezaji.
Amesema,kuimarika kwa utendaji pamoja na mambo mengine kumekuwa ni chachu ya mafanikio.
"Hata sasa sote tumeshuhudia kuongezeka kwa mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 7.9,”amesema Waziri Mkuu.
Pia ametoa wito kwa watendaji wote wa Sekta ya Madini kuongeza juhudi katika utendaji wao ili sekta hiyo iweze kuimarika zaidi na hatimaye iweze kuvuka lengo la asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo 2025 kama ilivyobainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Amesema kuwa, lengo la Serikali ni kutumia rasilimali ya madini kwa manufaa ya nchi na kuboresha uendeshaji wa shughuli za madini hapa nchini.
Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anapenda kuona sekta ya madini inakuwa nguzo muhimu ya uchumi wa nchi na ndio maana ameendelea kuipa umuhimu wa kipekee sekta hiyo kwa kutoa miongozo ambayo imeendelea kuiboresha sekta hiyo ya madini.
“Kipekee nimpongeze sana Rais kwa kuendelea kuhakikisha kuwa wadau wa sekta ya madini, wawekezaji na wachimbaji wadogo wanapata huduma kupitia maelekezo yake. Hii ni dhamira ya dhati ya Serikali yake ya awamu ya sita katika kukwamua na kuendeleza sekta hii,”amesema.
Waziri Mkuu ameipongeza Wizara ya Madini, kwa kuendelea kuandaa makongamano yanayowakutanisha wadau wa uchimbaji wa madini na Serikali, jambo ambalo limechangia kukua kwa sekta hiyo na kutoa wito kwa Wizara kuhakikisha, inaongeza jitihada na kupanua wigo wa ushirikiano baina ya wadau na Serikali.
Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Madini iendelee kuimarisha mifumo ya mawasiliano na wadau wa madini ili iweze kushughulikia kero zinazojitokeza na kuzitatua kwa wakati.
Amesema, Serikali itaendelea kuboresha taasisi zilizo chini yake ili ziweze kutoa huduma nzuri zaidi kwa wachimbaji ikiwa ni pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuendelea kuongeza mitambo ya kuchorongea miamba kwa ufanisi.
Akifungua Mkutano
Februari 22,2022 wakati akifungua Mkutano huo wa Nne wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika Sekta ya Madini.
Alisema,Sekta ya Madini ni moja ya sekta ya kipaumbele na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anafuatilia sana mijadala na mapendekezo yanayotolewa kupitia mikutano hiyo.
"Mikutano hii inasaidia kupokea maoni, michango na hivyo kuboresha mazingira ya uwekezaji,"amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko alisema,mkutano wa mwaka huu ni mwendelezo wa mkutano ulioanza mwaka 2019, lengo likiwa ni kujadili yanayotokea, "wapi tunakwama na tunasonga mbele. Matokeo yaliyotokea ni kipimo cha sababu ya kuendelea kukutana.
"Mikutano hii inaleta mitaji ya uwekezaji, tumehuhudia wengi wamejitokeza baada mikutano,"alisema Dkt.Biteko.
Aidha,Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini ni wazo lililobuniwa na Wizara ya Madini mwaka 2019 kwa lengo la kuwa na jukwaa la pamoja la kubadilishana uzoefu na kutambua fursa zilizopo na kupendekeza namna bora zaidi ya nchi inavyoweza kunuifaka na utajiri wa rasilimali zake.