NA DIRAMAKINI
BAADHI ya wawakilishi wa wananchi walioamua kuhama kwa hiari ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwenda Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamesema wameridhishwa na mazingira ya Kijiji cha Msomera na kuomba serikali kuboresha miundombinu iliyobakia.

Mkazi wa kata ya Ngorongoro Paul Mamasita ambaye amefika kijijini hapo kama muwakilishi wa kwenda kuangalia mazingira amesema ameridhishwa na uwekwaji wa huduma muhimu kijijini hapo,hasa majengo,miundombinu ya barabara na maji.
Ameongeza kuwa taarifa za awali waliambiwa kwamba Msomera kuna magonjwa ya mifugo,mazingira sio rafiki kwa makazi na ufugaji lakini imekuwa tofauti na walivyokuta kwani majani ya malisho yapo.
"Kulikuwa na upotoshaji kwamba mazingira sio rafiki lakini tumekutana na wenzetu wa kule ambao ni wenyeji,wameahidi kutugea ushirikiano na kuhusu maradhi ya mifugo ni yale yale yaliopo Ngorongoro na yanatibika hivyo tupo tayari kuhamia hapa na hakuna changamoto mpya kwetu,"amesema Mamasita.

"Msimamizi wa mradi ametuhakikishia kutajengwa shule mpya,kituo cha afya na miundombinu mingine na tumeona kwa macho yetu vipo baadhi,kwa hili tupo tayari kurudisha majibu na tutahamia Msomera,"amesema Emanuel.
Msimamizi msaidizi wa ujenzi wa nyumba hizo mhandisi Faudhi Seleman akizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Msomera amesema,kuna nyumba zipo tayari kabisa na wananchi wanaweza kuhamia muda wowote huku,nyingine zikimaliziwa sehemu ndogondogo.