*Abaini Meneja wa TANROADS Mkoa bado hajateuliwa
*Aliyemhamisha akutwa bado
yuko ‘site’ sababu ni mtaalamu wa madaraja
MOROGORO, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua
ujenzi wa barabara ya muda kwenye eneo la daraja la Kiyegeya na kusema kazi
inaenda vizuri sababu hakuna tena msongamano wa magari kama ilivyokuwa wiki
iliyopita.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesisitiza
kuwa Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa mikoa yote nchini wanapaswa
kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa madaraja yote siyo kwa juu tu bali hadi
chini ya madaraja ili kujiridhisha na usalama wake.
“Nilitoa agizo kwa mameneja
wa TANROADS ambao wana highways,
wazikague kila mara kwa sababu hatuhitaji kuwa na highways zilizobomoka.”
Waziri Mkuu ametoa agizo
hilo leo (Jumanne, Machi 10, 2020) wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, mara baada
ya kutembelea eneo hilo na kukagua ujenzi wa barabara ya muda ili kurejesha
mawasiliano na mikoa mingine.
“Nimekuja kuona kazi inaendeleaje,
nimekuta msongamano wa magari hakuna kama ilivyokuwa wiki iliyopita. Ile diversion
(barabara ya mchepuko) imesaidia kuondoa msongano uliokuwepo,” amesema Waziri
Mkuu.
“Mahitaji yetu ni kuwa na daraja
la kudumu, kwa hiyo mharakishe ujenzi wa daraja hilo, Mmesema sasa hivi mnapanga
kuweka daraja la zege ili maji yakija kwa wingi yaweze kupita juu ya hii barabara
ya muda, msisitizo ni kukamilisha kazi ya daraja la kudumu,” amesema wakati akizungumza
na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale.
Katika ukaguzi huo, Waziri
Mkuu alibaini kuwa Meneja wa TANROADS, mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin
Andalwisye ambaye aliagiza arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu
mwingine, bado alikuwepo kwenye eneo la tukio akiendelea na kazi.
Waziri Mkuu, KassimMajaliwa akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS,
Mhandisi Patric Mfugale (mwenye kofia) wakati alipokagua ujenzi wa
barabara ya muda katika eneo la Kiyegeya wilayani Kilosa Machi 10,
2020. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel
Kalobelo. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Uamuzi niliochukua wa
kumhamisha Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro ulikuwa sahihi kwa sababu huyu
Bwana anaonekana hawezi kazi ya kusimamia wengine. Fedha ya ukaguzi ipo, ya
ujenzi ipo, halafu kazi haifanyiki. Kazi ya kusupervise haiwezi, kwa hiyo, ateuliwe
Meneja mwingine,” alisisitiza.
“Nilimuuliza meneja
aliyekuwepo kama wana fedha za ukaguzi, akasema anayo. Nikamuuliza kama anayo
fedha ya spot maintenance, akasema
anayo. Fedha hizi zote zilipaswa zitumike kwa kazi iliyopangwa, lakini hilo
halikufanyika.”
Akijibu hoja hiyo, Mhandishi
Mfugale alisema amemuacha Mhandisi Godwin Andalwisye aendelee kuwepo pale site kwa sababu ya utalaamu wake kweye
madaraja. “Ulishatoa maelekezo kuwa aondolewe, na wa kumhamisha ni mimi,
tunatumia tu utaalmu wake.
Alipoulizwa kama ameshateua Meneja
mwingine wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mfugale alikiri kwamba bado hajamteua
mtu mwingine.
Jumatano iliyopita, (Machi 4,
2020) Waziri Mkuu alikatisha ziara yake mkoani Tanga na kutembelea eneo hilo ambako
alishuhudia mlundikano wa magari na abiria hali ambayo haikumfurahisha.
Aliagiza Meneja wa Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye arejeshwe
wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine mara moja kwa sababu ya kuzembea
kutimiza wajibu wake.
Waziri Mkuu ambaye alisafiri
kwa magari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, pia alisimama Morogoro na kukagua
ujenzi wa uzio wa makaburi ya Kola Hill ambako walizikwa wahanga wa ajali ya lori
la mafuta lililopinduka na kulipuka Agosti 10, 2019 na kuua watu 115, kati yao wanaume
walikuwa ni 109 na wanawake ni sita.
Akiwa
makaburini hapo, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Morogoro uweke
utaratibu wa kuwa na mtu maalum atakayesimamia masuala ya mazishi yote
yatakayofanyika kwenye makaburi ya Kola Hill.
Amesema mtu
huyo ahakikishe makaburi yote yanachimbwa katika utaratibu na mpangilio
utakaoliwezesha eneo hilo kuwa na nafasi ya kuzika watu wengi. “Utaratibu wa
sasa wa kuchimba makaburi kiholela utalifanya eneo hili lijae haraka huku
likiwa halina mpangilio maalum.”
Waziri Mkuu pia
aliridhia maombi ya uongozi wa mkoa wa Morogoro ya kutaka akubali makaburi
hayo yajengewe ili yawe na muonekano mzuri kazi ambayo itagharimu zaidi ya
sh. milioni 12.
Uongozi huo pia
uliomba rdhaa ya Waziri Mkuu kutengeneza mandhari ya ndani ya uzio (Landscaping)
kazi ambayo itagharimu sh. 1,682,500/- pamoja na kujenga mnara wa kumbukumbu
kwa gharama ya sh. 4,173,125/-.
Tags
Habari