Ripoti hiyo inaeleza kuwa Wakenya 435,000 wamepoteza kazi kutokana na athari za kiuchumi za janga la Covid-19, hali ambayo imewaacha wengi wakiwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.
Sekta ambayo imeathiriwa zaidi ni utalii na hoteli ambayo imewaajiri watu 1.6 milioni lakini wengi sasa wamefutwa kazi huku wengine wakipewa likizo bila malipo.
Katika sekta ya maua, vibarua 30,000 wamefutwa kazi huku wafanyikazi 40,000 wakipewa likizo bila mshahara.
Kwa jumla, yasema ripoti hiyo ya Scanad, asilimia 54 ya walioajiriwa kazi nao wamekatwa mishahara, jambo ambalo limepunguza uwezo wao wa kifedha.
Matatizo haya yamefanya karibu ya nusu ya Wakenya (asilimia 47) kutegemea misaada ya chakula kutoka kwa watu wa familia zao ama wahisani.
Nayo asilimia 63 wanakumbwa na matatizo ya kulipa kodi za nyumba, asilimia 67 wanashindwa kulipia huduma kama za maji, stima na televisheni huku asilimia 75 wakilemewa kulipa madeni, ripoti hiyo inasema.
Utafiti huo unaeleza kuwa watu wa mapato ya chini wamepata pigo kubwa zaidi na wengi sasa wanategemea misaada ya chakula kutoka kwa familia na wengine wamehamia makazi ya jamaa zao baada ya kushindwa kulipa kodi.
Familia nyingi, inaeleza ripoti hiyo, sasa zinakula chakula mara moja kwa siku hasa uji kutokana na uhaba wa fedha.
Nao wakazi wengi wa mijini walipeleka watoto wao mashambani kuishi na wazazi wao. Lakini kwa upande mwingine, athari za Covid-19 kwa matajiri ni kutatizwa kwa maisha yao lakini kifedha bado hawajatingizwa.
Wakati huo huo, wakazi wa eneo la Mlima Kenya wanaogopa zaidi ugonjwa wa Covid-19 kuliko maeneo mengine nchini, ripoti ya utafiti wa shirika la TIFA imefichua.
Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa Alhamisi, asilimia 72 ya wakazi waliohojiwa Mlima Kenya walikiri kuogopa ugonjwa huo zaidi.
Maeneo mengine yenye yenye wakazi wengi wanaoogopa maambukizi ya Covid-19 ni Mashariki (asilimia 69), Nyanza (67), Pwani (64) na Nairobi (52).
Kwa jumla, utafiti huo ambao uliendeshwa kati ya Juni 7 na Juni 21, 2020, umebainisha kuwa asilimia 65 ya Wakenya wanahofia kuambukizwa Covid-19. Na asilimia 16 ya Wakenya hawana wasiwasi wowote.
Jumla ya watu 843 walihojiwa katika utafiti huo ambao uliendeshwa katika maeneo yote nane nchini ambayo zamani ilijulikana kama mikoa.
Utafiti huo pia uligundua kuwa asilimia 79 ya waliohojiwa wako tayari kujiwasilisha kwa upimaji kubaini ikiwa wana virusi vya corona, na asilimia 10 walisema hawako tayari kupimwa.
Kati ya wale ambao wako tayari kupimwa hata hivyo wanahofia kuwa shughuli hiyo ni uchungu na kando na kuogopa kupelekwa katika vituo vya kujitenga pamoja na kutengwa na majirani.
Miongoni mwao wale ambao hawako tayari kujitoza kupimwa corona, asilimia 39 wanasema shughuli hiyo inasababisha usumbufu, asilimia 10 wanasema wanahofia kuwekwa karantini huku asilimia nane wanasema hawataki kupimwa kwa hofu ya kutengwa na majirani zao endapo watapatikana na virusi hivyo.