"Wananchi wakitupatia ridhaa ACT Wazalendo tunakwenda kuunda Serikali itakayosimamia uhuru, haki na demokrasia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania"
Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe ameyabainisha hayo leo jijjni Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Ilani ya uchaguzi wa chama hicho uliofanyika jijini humo.Amesema kuwa, ilani waliyoizindua imegusa maeneo yote muhimu yanayogusa moja kwa moja maisha ya Mtanzania hususani maskini katika maeneo yote ya nchi.
Zitto amesema kuwa, kama ACT-Wazalendo kitashinda Uchaguzi Mkuu Serikali yake itasimamia uhuru, haki na demokrasia kwa kufuta sheria kandamizi pamoja na kuanzisha timu ya majaji kwa ajili ya kuchunguza matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Naye Mshauri wa chama hicho na Mgombea Urais, Bernard Membe akizungumza mara baada ya kukabidhiwa rasmi ilani hiyo amesema kuwa, ana imani kubwa ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 kutokana na mpasuko uliopo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Vipaumbele vingine ni kilimo cha kimapinduzi na mazingira wezeshi ya biashara, usawa na ustawi wa wanawake na vijana, hifadhi ya jamii kwa kila mtu.
Hii inamaanisha afya bora kwa wote, ushirika wa kisasa kwa maendeleo jumuishi, haki za watu wenye ulemavu, maji safi, salama na gharama nafuu na ajira mpya milioni 10.
Tags
Siasa