Benki ya NMB Plc yamtangaza Ruth Zaipuna kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu mpya

 BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB Plc imemtangaza Ruth Zaipuna kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa benki hiyo uteuzi ulioanza leo Agosti 18,2020, anaripoti Mwandishi Maalum kutoka Dodoma.

Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Plc,Dkt. Edwin Mhede amemtangaza Zaipuna huku akikiri kuwa mchakato wa kumpata haukuwa mwepesi, lakini hakukuwa na upendeleo isipokuwa walitazama wasifu, utendaji na maslahi ya benki na Tanzania.

Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Plc,Dkt. Edwin Mhede akimpongeza Ofisa Mtendaji Mkuu mpya, Ruth Zaipuna.

Dkt.Mhede amesema, katika kipindi kirefu benki hiyo ilikosa mtu baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake kuondoka na hivyo walibaki na mtu aliyekuwa anakaimu kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, lakini takwa la kisheria lilikuwa linawabana kuwa ni lazima wapate mtu.

Zaipuna anakuwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu benki hiyo ilipobinafsishwa ambapo kwa nyakati zote nafasi za juu zilishikwa na wageni wakiwemo Ineke Bussemaker aliyekuwa Mkurugenzi tangu 2014-2018 kisha nafasi hiyo ikachukuliwa na Albert Jonkergow ambaye alishikiria kwa kipindi cha mpito cha miezi sita kabla ya Zaipuna kupewa nafasi ya kukaimu.

Mwenyekiti amesema, mchakato wa kumpata Mtendaji Mkuu ulikamilika Juni 30,2020 na leo ilikuwa ni siku ya kumtangaza huku akibainisha kuwa sifa zote zilizotakiwa katika nafasi hiyo, wamejiridhisha kuwa Zaipuna anazo hivyo hakuna shaka kuhusu utumishi wake katika nafasi hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Plc,Dkt. Edwin Mhede akimpongeza Ofisa Mtendaji Mkuu mpya, Ruth Zaipuna.

‘’Katika kipindi chote tulihangaika kumpata mtu mwenye kufikia vigezo vinavyotakiwa, lakini wakati mwanamama huyu alipokuwa anakaimu, benki imeendelea kufanya vizuri zaidi na kukuza mtaji wake, hakuna mahali paliyumba chini ya usimamizi wake,hivi kwa hali hiyo mnadhani tungefanyaje,’’amesema Dkt.Mhede.

Ametaja mafanikio makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa kukaimu kwa ofisa huyo ni faida kubwa ambayo benki imekuwa ikipata ikiwemo shilingi Bilioni 93 zilizopatikana katika kipindi cha nusu ya kwanza ya 2020 huku mahusiano yakizidi kuimarika kati ya benki na Serikali pamoja na wateja wake.

Hata hivyo alimuagiza mtendaji huyo kuhakikisha benki inaendelea kuwa imara na yenye kutoa matumaini kwa wananchi wake huku akisisitiza ushirikiano wa timu moja kati ya kiongozi huyo na watumishi wengine ndani ya taasisi yao.

Akizungumza mara baada ya kupokea uteuzi huyo, Zaipuna amesema ni uteuzi wa ushindi kwa NMB wala siyo yeye, lakini ameahidi kwamba atakuwa mtumishi kama ilivyo kwa watumishi wengine kwani anaamini kila mmoja anamchango wake kwa nafasi yake, hivyo ameomba wenzake kujitoa zaidi katika kuwahudumia Watanzania.

Zaipuna ametaja vipaumbele vitano atakavyoanza navyo ikiwemo NMB kuendelea kukua kila mwaka na kuwa benki namba moja nchini,benki kuendelea kuwa chaguo la wateja, kuongeza na kuimarisha ushirikiano kwa wateja na watumishi na kipaumbele cha tano ni kuendelea kuboresha maslahi kwa watumishi ili vijana wa Kitanzania wavutiwe na kutamani zaidi waajiriwe NMB.

Amesema hayo yote yatawezekana ikiwa kila mtumishi atakuwa na nidhamu ya utekelezaji na kujituma katika ubunifu wa ushirikishwaji wa mipango, lakini kwa upande wake amesema ataendeleza kasi iliyopo ili misingi iliyojengwa isiyumbe.

Kuhusu wanahisa ameitaja Serikali ya Tanzania na wabia wa Benki ya Rabo ya Uholanzi kwamba waondoe hofu kuhusu NMB kwani ni chombo kilichosimama kwa ajili ya kutoa matumaini kwa watu hivyo wataendeleza kasi hiyo wakati wote.

Awali, Mjumbe wa Bodi, Margaret Ikongo amewataka wajumbe kutoa ushirikiano mkubwa kwa CE0 wao mpya kwa kuwa kazi anayokwenda kuifanya ni kubwa na ndiye mbeba maono wa chombo hicho, hivyo ushindi wake utategemea nguvu ya pamoja na watumishi ikiwemo kumuombea.

Ikongo amemtaka Zaipuna kufanya kazi kwa kuwashirikisha zaidi watumishi wenzake na atambue kuwa kila mmoja ana mchango mkubwa kwa sehemu yake, lakini akaomba watumishi kumuombea kiongozi huyo katika cheo hicho kipya alichokabidhiwa.

 

Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com

 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news