TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka leo inawafikisha mahakamani watuhumiwa watano kwa tuhuma za rushwa, uhujumu uchumi na ukwepaji kodi wa kiasi cha shilingi 153,543,550, anaripoti MWANDISHI WETU,www.diramakini.co.tz
Doreen J.Kapwani ambaye ni Afisa Uhusiano wa TAKUKURU kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Brigedia Jenerali John Mbungo ameyabainisha hayo leo.
Amesema, kati ya watuhumiwa hao, watuhumiwa wanne walikuwa ni watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Kigoma ambao tayari wamefukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria.
Kapwani amesema, mtuhumiwa mmoja ni Mkurugenzi wa Kampuni yua M/S Saxon Building Contractors Limited ambayo ilipewa zabuni ya ujenzi wa gati la Sibwesa katika Ziwa Tanganyika.
"Majina ya watuhumiwa hao ambao wote watafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma leo ni Rodrick Ndeonasia Uiso ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Saxon Building Contractors Limited, Ajuaye Kheri Msese aliyekuwa Meneja Bandari ya Kigoma, Herman Ndiboto Shimbe aliyekuwa Afisa Uhasibu TPA Kigoma, Jesse Godwin Mpenzie aliyekuwa Mhandisi Mkazi TPA Kigoma, Lusubilo Anosisye Mwakyusa aliyekuwa Afisa Rasilimali watu TPA Kigoma.
"Uchunguzi wa TAKUKURU umebaini kwamba, watuhumiwa hawa kwa pamoja wamehusika kutenda makosa ya rushwa na uhujumu uchumi yakiwemo kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo,ukwepaji kodi, kuisababishia mamlaka hasara pamoja na utakatishaji fedha haramu,"amefafanua.
Kapwani anasema, sambamba na kuwafikisha watuhumiwa hao watano mahakamani leo, uchunguzi wa TAKUKURU bado utaendelea kwa lengo la kubaini kiasi cha fedha zilizohujumiwa ikiwa ni pamoja na kumtafuta na kuchukua hatua za kisheria mtuhumiwa mwingine aitwaye Madaraka Robert Madaraka aliyekuwa Mhasibu katika Bandari ya Kigoma ambaye amehusika katika tuhuma hii, ili naye aweze kuunganishwa katika shauri hili.
"Tunawaomba wananchi, kwa yeyote atakayekuwa na taarifa za kupatikana kwa mtuhumiwa huyu (Madaraka Robert Madaraka) tafadhali atoe taarifa ofisi yoyote ya TAKUKURU iliyopo karibu naye,"amesema Kapwani, www.diramakini.co.tz
Tags
Habari