DOKTA MABULA: ITUMIENI MICHEZO KUIMARISHA AFYA, KUONGEZA UFAHAMU

WANAFUNZI na walimu wa shule za msingi na sekondari kwa Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza wametakiwa kutumia michezo kwa ajili ya kuimarisha afya zao dhidi ya magonjwa na kuongeza ufahamu kwa watoto, hivyo kuchochea ufaulu,anaripoti MWANDISHI WETU,www.diramakini.co.tz

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula katika viwanja vya Shule ya Msingi Sabasaba wakati akifungua mashindano ya MWAOMI Inter School Sports Competition yanayohusisha shule za sekondari na msingi za ndani ya manispaa hiyo yanayotegemewa kufika tamati Septemba 19,mwaka huu.

Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akiwahutubia wakati wa ufunguzi huo.

Dkt.Mabula amesema kuwa, Serikali imedhamiria kukuza michezo kwa kushirikiana na wadau kwa kuhakikisha wanajenga na kuimarisha miundombinu kwa ajili ya michezo, hivyo kuwaomba kuitumia kwa kuimarisha afya za watoto na kuwa kishawishi cha kuongea ufaulu katika masomo yao kwa kutenga muda wa michezo na kujifunza

"Mlezi wa Wilaya ya Ilemela na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu anatuhimiza kufanya mazoezi, Na kama mnavyojua michezo ni sehemu ya mazoezi, Tuitumie kwa ajili ya kuimarisha afya zetu,"amesema.

Pia Dkt.Mabula ametumia fursa hiyo kuipongeza Manispaa ya Ilemela chini ya Mkurugenzi wake, Ndugu John Wanga kwa kukubali viwanja vya shule zake kutumika kwa shughuli za michezo sanjari na kuwakaribisha wadau wa maendeleo na kuwaahidi ushirikiano katika kuhahakisha sekta ya michezo inaendelezwa.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Mratibu wa Shirika la MWAOMI, Ndugu Fredrick Eliachim Rubinda mbali na kuelezea historia ya mashindano hayo akabainisha faida mbalimbali watakazopata washiriki ikiwemo kujenga afya za miili yao, kuimarisha ubongo, kuwaepusha na kujiingiza katika matendo ya uvunjifu wa sheria na yasiyofaa kama uasherati na matumizi ya dawa ya kulevya.

Naye Afisa Michezo wa Manispaa ya Ilemela, Mwalimu Bahati Sosho Kizito amesema kuwa, licha ya wilaya yake kuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya elimu na michezo bado inakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya michezo, hivyo kuwaomba wadau kuzidi kujitokeza kupambana na changamoto hiyo.

Akihitimisha mmoja wa wanafunzi wanaoshiriki mashindano hayo, Salma Yahya kutoka Shule ya Sekondari Lumala ameshukuru kwa uwepo wa michezo hiyo kwani ni muda mrefu wamekuwa na likizo ya kimichezo kutokana na ugonjwa wa homa ya mafua makali wa Covid-19.




Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news