Emirates warejesha huduma za usafiri wa anga kwa kishindo, Dubai yafungua milango kwa wafanyabiashara, watalii wote,

SHIRIKA la Ndege la Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) la Emirates ambalo linaloongoza kwa huduma bora Kimataifa limeendelea kufungua anga katika miji mbalimbali duniani ikiwemo Afrika ikiwa ni sehemu ya kutoa huduma za safari ambazo zilisimama kufuatia mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika hilo ambayo imeelezwa kuwa, huduma katika miji ya Conakry, Guinea na Dakar, Senegal zimerejeshwa na zitaanza rasmi Septemba 3, mwaka huu, na hii itafanya idadi ya miji ambayo inahudumiwa na shirika hilo barani Afrika kufikia nane.

Kwa mujibu  wa taarifa hiyo,safari kutoka Dubai kwenda Conakry na Dakar zitakua mara mbili kwa wiki kupitia Boeing 777-300ER.

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa,kupanuka kwa mtandao huo wa anga kumepeleka ongezeko la kufikia miji 77 zaidi inayohudumiwa na shirika hilo la Kimataifa katika safari za anga.

Aidha,shirika hilo limeendelea kuunganisha watu kutoka sehemu mbalimbali duniani ikiwemo kutoka Mashariki ya Kati, Ulaya, Afrika, Amerika, na Mashariki ya kati kupitia Dubai na hiyo ni kutokana na huduma zao ambazo huwawezesha wateja kuweka machaguo yao ya safari kupitia shirika hilo au mawakala wake.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa,baada ya Mji wa Dubai kufunguliwa kwa shughuli za biashara za Kimataifa na utalii wateja wanaweza kuutembelea na wakiwasili suala la kupima Covid-19 ni lazima kwa wasafiri wanaowasili Dubai na UAE wakiwemo raia wa UAE na watalii bila kujali nchi walizotoka.

Imeelezwa kuwa, sehemu zote zinazopendwa kutembelewa Dubai zikiwemo fukwe mbalimbali, sehemu za michezo na maonesho mbalimbali tayari zimefunguliwa na watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani wanaweza kuzitembelea.

Ikumbukwe kuwa Dubai ni moja ya sehemu inayopendwa kutembelewa na watu wengi duniani, na kwa mwaka 2019 mji huo ulikaribisha wageni milioni 16.7 ambao waliunganishwa na Emirates, ambalo ni shirika kubwa la ndege duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news