Habari Development Association yatoa tamko kwa wanasiasa wanaotoa kauli za kichochezi kuelekea Uchaguzi Mkuu

TASISI ya Habari Development Association imesema imestushwa na matamshi yanayoendelea kutolewa na baadhi ya wanasiasa  wa vyama vya upinzani wakiwemo baadhi ya wagombea nafasi ya urais, ubunge na udiwani ambayo yanahatarisha amani ya nchi hususani kwenye kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28,mwaka huu.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo na Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo, Bernard James kwa niaba ya viongozi wenzake.

James amesema, ni vema wanasiasa na wagombea wa nafasi mbalimbali wakiwemo wagombea  urais  kuchunga ndimi zao, waache kutoa maneno ya uchochezi ya kuwagawa Watanzania.

"Kwa mfano mgombea urais wa CHADEMA Tundu Lissu alipokuwa akihutubia kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho ambao ulimpitisha kuwa mgombea uliofanyika Agosti,mwaka huu jijini Dar es salaam, alinukuliwa akisema “uhuni sasa basi” .

"Pia amenukuliwa kwenye mikutano yake wakati akizunguka mikoani akitafuta wadhamini akisema kuwa akishindwa uchaguzi atahamasisha wafuasi wake na wananchi waingie barabarani.Aidha mara kadhaa akihamasisha wagombea wachukue na  kurudisha fomu kwa maandamano na kutishia kwamba maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wasipokuwepo Ofisini, Ofisi zao zitakuwa halali yao. Huyu ni mgombea ambaye amekuwa akitoa  matamshi hayo  kwenye mikutano yake mbalimbali,"amesema wakati akisoma tamko lao la kuhamasisha amani na utulivu .

Aidha, amesema kuna mgombea mwingine wa urais upande wa Zanzibar anayewakilisha  Chama cha ACT Wazalendo,Maalim Seif Sharif  Ahmad  amekuwa akitoa matamshi kuwa safari hii hatakubali kushindwa  tena na anahamasisha wapiga kura kulinda kura kwa silaha za jajadi.

"Pia anadai kuwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni matawi ya CCM, kitu ambacho sio kweli.Ipo mifano mingi ya viongozi hasa wa upinzani ambao wamekuwa matamshi ambayo hayana muelekeo mzuri.

"Kwa hata kauli ya Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyoitoa hivi karibuni jijini Dar es Salaam akidai kuna wagombea ubunge wa chama chake wametekwa na kuteswa na utekaji huo ni wa kisiasa na unafanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

"Ushauri wetu kwa kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo ni kuwa angesubiri vyombo vinavyofanya uchunguzi wa jambo hilo vikamilishe kazi yake.Kauli hiyo ya Zitto inaweza kuibua chuki baina ya wanachama wa vyama vya siasa na hivyo kuleta vurugu hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu,"amesema James.

Kupitia tamko hilo, James amesisitiza kauli hizo ni za hatari na zinahatarisha amani ,utulivu na umoja wa Taifa letu uliojengwa na waasisi wa taifa letu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Amri Abeid Karume

Aidha, wamekuwa  wakishuhudia  matamshi ya shari yakitolewa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA akiwemo  mgombea wa ubunge Jimbo la Iringa Mjini, Peter Msigwa katika mikutano yake  ya hivi karibuni kwani matamshi mengi yaliyotolewa hayakuwa ya staha.

"Tunawasihi wagombea hao kuzingatia sheria za nchi yetu wakati wote wa kampeni na baada ya matokeo kutangazwa na hivyo waache kutoa kauli za shari vinginevyo nchi yetu inaweza kuingia kwenye machafuko na vurugu  kama ilivyowahi kutokea kwenye nchi za jirani.

"Tunawauliza wanasiasa wetu  je, wanapenda yaliyotokea  huko  yatokee nchini mwetu?  Ni dhahiri hali kama hiyo inapotokea waathirika ni wananchi, hususani akina mama, wazee na watoto.

"Tunatoa mwito kwa wananchi pamoja na wanachama wa vyama vyote vya siasa kupuuza kauli hizo zinazotolewa na baadhi ya wagombea ili kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu kwa sababu machafuko yakitokea  wao ndio watakao athirika,"amesisitiza.

Wakati huo huo taasisi hiyo imewashauri waliokuwa wagombea katika hatua ya awali ya uchaguzi ndani ya CCM ambao hawakufanikiwa kupitishwa na vikao vya chama hicho kuwa wawe na subira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news