LATRA yafungua dirisha la kupokea maoni mapendekezo ya nauli usafiri wa treni Moshi-Arusha

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Gilliard Ngewe amewataka wananchi kuandika kwa maandishi maoni yao ndani ya siku saba na kuyawakilisha kwake kabla ya Septemba, mwaka huu li yawe sehemu ya mchakato wa kutambua mapendekezo ya Shirika la Reli nchini (TRC) kuhusu nauli zilizopendekezwa kwa usafiri wa treni wa Arusha kwenda Moshi.
Wadau wa treni ya abiria ya Moshi - Arusha wakiwa katika mkutano wa kujadili na kupendekeza bei za nauli, mkutano uliofanyika jijini Arusha.

Ngwewe ameyasema hayo katika mkutano wa wadau wa treni ya abiria ya Arusha kwenda Moshi uliofanyika jijini Arusha ambapo amesema kila mwananchi amepewa nafasi ya kutoa maoni yake kuhusu nauli elekezi itakayotumika katika usafiri wa treni.

Amesema kuwa, mkutano huo ni mahususi kwa ajili ya kukusanya mapendekezo kutoka TRC wanaotaka nauli za huduma ya usafiri kwa abiria kutoka Arusha kwenda Moshi pamoja na wadau wa usafiri huo kutoa maoni na mapendekezo yao ili kwa pamoja waweze kuweka bei ya nauli ambayo itakuwa nafuu kwa kila mmoja.

Awali akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,Richard Kwitega amesema takribani miaka 30 imepita usafiri wa treni ulisitisha safari zake hivyo ni wakati sasa kuchangamkia fursa ya usafiri huo kwani utakuwa rahisi na bei nafuu kwa mtanzania.
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega akifungua mkutano wa wadau wa Treni ya abiria Moshi-Arusha.
Kwa upande wao wadau wa usafiri wa treni mkoani Arusha wameliomba Shirika la Reli Tanzania kuboresha bei za nauli katika kila daraja ili kumfikia kila moja kwenye usafiri huo sambamba na kuwajali watu wenye mahitaji maalum.

Akizungumza kwa niaba ya wadau hao,Mwenyekiti wa Wasafirishaji Mkoa wa Arusha,Adolfu Massawe amesema, ujio wa treni hiyo utarahisisha usafirishaji wa mizigo kwa wafanyabiashara watakaotumia usafiri huo na kufanya kufanya biashara kwenda vizuri pia hautaathiri usafiri wa magari ya abiria kwani njia zipo nyingi tofauti na njia ya treni ambayo iko moja tu.

Naye Amina Njoka ambaye ni Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Arusha amesema, kama wamachinga wamefurahishwa na ujio wa usafiri huo kwani unarahisisha gharama za uletaji wa bidhaa zao ambapo amewataka wafanyabiashara wadogo kutumia fursa hiyo katika kusafiri na kufuata mizigo yao sehemu mbalimbali.

Akizungumzia ushirikishwaji wa upangaji wa bei za nauli Amina amesema kuwa, ni mwafaka mzuri kwa wafanyabiashara kushirikishwa katika upangaji wa nauli kwani wanafahamiana wao kwa wao kutokana na mitaji yao, kwani kabla ya ujio wa treni hiyo walikuwa wanakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa za nauli.

Pia TRC imetoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya nauli kwa abiria ambayo nauli kwa watu wazima kwa daraja la pili itakuwa shilingi 2,000,daraja la tatu shilingi elfu 1500 huku watoto ikiwa shilingi 400.
Kaimu Katibu Mtendaji LATRA CC,Fatuma Kulita akiwasilisha maoni na mapendekezo ya bei kwa wasafiri  wa treni katika mkutano wa wadau wa treni ya abiria ya Moshi-Arusha  uliofanyika jijini Arusha.

Aidha,Kaimu Katibu Mtendaji kutoka Baraza la Ushauri la Utumiaji wa Usafiri wa Ardhi (LATRA CC),Fatuma Kulita ametoa maoni juu ya miudombinu ya TRC kuzingatia matakwa ya abiria ili kuweka ushindani na usafiri wa mabasi na kupata wateja wengi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news