ZAIDI ya watu 200,000 nchini Sudan wanakabiliana na hali ngumu ya maisha baada ya makazi yao na mali kuharibiwa vibaya na mvua mfululizo ambazo zinaendelea kunyesha tangu Julai, mwaka huu.
Mvua hizo zimesababisha mafuriko hatarishi kwa maisha ya watu katika majimbo zaidi ya 15 huku Jimbo la White Nile lilopo Kusini mwa nchi hiyo likiwa limeathirika vibaya.
Mkazi
wa Al-Ikmayr mjini Omdurman, Khartoum nchini Sudan akijaribu kuyaondoa
maji kutoka Blue Nile ambayo yalifurika katika makazi yake. Picha na
Reuters. |
Hayo yanajiri ingawa Ethiopia imeanza kujaza maji katika bwawa la Renaissance ( An Nahadhah) katika Mto Nile licha ya kuwepo mvutano baina ya mataifa hayo ikiwemo Misri kuhusiana na zoezi hilo. Inaelezwa, hatua hiyo ya Ethiopia inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa Sudan kudhibiti mafuriko siku za usoni.
Kutokana na hali hiyo, Umoja wa Matafa umebainisha kupitia taarifa yake ya karibuni kuwa, zaidi ya makazi 37,000 yameathiriwa vibaya huku mvua hizo za masika zikitajwa zitaendelea hadi Oktoba mwaka huu na zinatajwa kuwa za viwango vya juu tofauti na miaka mingine.
Pia maafisa wa Sudan wametangaza kuwa, hasara zinazotokana na mvua hizo zimeongeza tishio zaidi nchini humo kwa upande wa afya, watu kufariki, makazi na mali kuharibika kwani hata Mto Nile umefurika.
Waziri wa Umwagiliaji na Vyanzo vya Maji wa Sudan,Yassir Abbas amekaririwa akisema kuwa, kiwango cha maji katika Mto Blue Nile kipo juu zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kamati ya Kupambana na Maafa ya Mafuriko katika Wizara ya Maji ya Sudan,Abdulrahman Saghiroun ameeleza kuwa, kiwango cha maji katika Mto Nile kinatarajiwa kuongezeka zaidi katika siku zijazo.