WANANCHI wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli kwa kuwaondolea kero ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma ya majisafi na salama, anaripoti Mohamed Saif kutoka Magu...
Shukrani hizo wamezitoa wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ya kukagua mradi wa maji wa Matela katika Kijiji cha Matela wilayani humo.
Aweso amesema ziara yake imelenga kutembelea miradi ambayo wakandarsi wake wamechelewa kuikamilisha kwa wakati kama inavyoelekeza mikataba yao.
Amebainisha kuwa, Matela ni miongoni mwa miradi uliyoisumbua Wizara ya Maji, kwani ujenzi wake ulichukua muda mrefu na hivyo kuwacheleweshea wananchi kupata huduma ya maji kinyume na azma ya Rais Dokta John Magufuli.
Naibu
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto) akimsikiliza mkazi wa Kijiji cha Matela,
Naombi Mbotela akieleza adha waliyokuwa nayo kabla ya kujengewa mradi wa maji.Picha na Mohamed Saif.
“Tangu anaingia madarakani, Rais Magufuli aliazimia kuwaondolea kero ya maji wananchi wake, kuna baadhi ya miradi inakwamisha azma hiyo kufikiwa kwa wakati ukiwemo huu wa Matela ambao hata hivyo nafarijika kuona sasa nao umekamilika,”amesema Aweso.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Naibu Waziri Aweso, wananchi wa Matela wamesema licha ya kwamba mradi huo umechelewa kukamilika kwa wakati, lakini umeleta faraja katika maisha yao.Naomi Mbotela mkazi wa Kijiji cha Matela amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia mradi huo ambao amesema umewaondolea kero ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kufuata huduma ya maji.
Wananchi
wa Kijiji cha Matela wilayani Magu wakifurahia mradi wa maji wakati wa ziara
ya Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani) kwenye mradi huo.Picha na Mohamed Saif.
“Kwa sasa hatuna shaka kwenye suala la maji, zamani sisi wanawake tuliteseka sana, tulikua tunatoka saa 11 alfajiri na kutembea umbali mrefu kufuata maji na hii wakati mwingine ilitusababishia migogoro kwenye ndoa zetu,”amesema Mbotela.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Matela, Elias Njita alisema uwepo wa mradi huo ni uthibitisho kuwa Rais. Dkt Magufuli ni Rais wa wanyonge.
“Tunamshukuru sana Rais kutuona na kutujali sisi wanyonge huku vijijini, ametoa fedha nyingi kutujengea huu mradi ili sisi wanyonge tupate maji,”amesema Njita.
Ameahidi kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli hasa ikizingatiwa kwamba kwa muda mrefu wananchi wa maeneo ya vijijini wamekuwa wakisahaulika.
“Tunaahidi sisi tutamuunga mkono Rais, tunaahidi hatutomuangusha kazi anayofanya ni kubwa na ni ngumu sisi wanyonge tulikuwa tumesahaulika, lakini yeye anatujali ili na sisi tuweze kujikwamua kimaendeleo,”ameongeza Njita.Meneja wa RUWASA Wilaya ya Magu, Mhandisi Anna Mbawala (katikati) akiwasilisha taarifa ya mradi wa Matela kwa Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani). Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli na kulia ni Meneja RUWASA Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Immaculata Raphael. (Picha na Mohamed Saif.
Aidha, kwa mujibu wa msimamizi wa mradi Meneja wa Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilayani Magu, Mhandisi Anna Mbawala ni kwamba ulianza kutekelezwa na Mkandarasi M/S STC Construction Company Ltd Mwaka 2017 na ulipaswa kukamilika 2019 na kuwa umetekelezwa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) kwa gharama ya shilingi milioni 397.9.
Alibainisha kwamba, ulianza kutoa maji rasmi Agosti 2, 2020 na kuwa umekabidhiwa kwa Jumuiya ya Watumiaji Maji ya Nyanguge-muda kwa ajili ya kuhudumia wakazi wapatao 5,000 wa Kijiji cha Matela na vitongoji vyake.
Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com