Mahakama ya Mafisadi yang'ata vigogo

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Mafisadi) imemuhukumu aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya (70) na wenzake wanne kulipa fidia ya sh. bilioni 1.5 baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na kukiri makosa yaliyokuwa yanawakabili.

Aidha,Mahakama hiyo imewataka washtakiwa hao kila mmoja kulipa faini ya shilingi milioni 1,000,000 au kwenda jela miezi sita kwa kukiri mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya dola za Kimarekani milioni 6,000,000.

Picha na Mtandao.

Washitakiwa wengine mbali na Harry Kitilya ni maafisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare (44), Sioi Salomon (44), Kamishina wa Sera ya Uchunguzi wa Madeni kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Benason Shallanda (59) na Msaidizi wake Alfred Misana (50).Hukumu hiyo imesomwa na Jaji Immaculata Banzi ambapo mapema kabla ya kusomwa kwa adhabu, DPP Biswalo Mganga alidai kuwa alipokea barua ya washtakiwa wakiomba kuingia makubaliano ya kukiri makosa yao na kwamba baada ya majadiliano amewafutia washtakiwa hao mashtaka 57 kati ya 58 waliyokuwa wanakabiliwa nayo.

Hivyo, aliiomba Mahakama kuyapokea makubaliano hayo na kuyasajili kwa mujibu wa sheria na upande wa utetezi haukuwa na pingamizi.

Kufuatia taarifa hiyo, mahakama imeyapokea makubaliano hayo kwa mujibu wa kifungu cha 194 (D) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 ambayo inaelekeza kila mshitakiwa ahojiwe na mahakama ichukue majibu yake.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, DPP Mganga alidai hawana rekodi ya makosa ya nyuma ya washtakiwa hivyo, aliomba kwa mujibu wa makubaliano washitakiwa walipe shilingi bilioni 1.5 kama fidia ya hasara waliyosababisha.

Katika utetezi wao washtakiwa kupitia jopo la mawakili waao wakiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa walidai, washitakiwa ni wakosaji wa kwanza na kwamba mshitakiwa  Harry Kitilya ni mzee na anakabiliwa na maradhi mbalimbali, hivyo hayupo vizuri kiafya.

Amedai kuwa, washitakiwa wote wana familia zinazowategemea na kitendo cha kukaa rumande kwa miaka minne na nusu, familia zao zilikuwa kwenye mahangaiko ya kimya kimya.

Pia amedai kuwa, kukiri kwao makosa kumeokoa rasilimali fedha na muda wa Mahakama, pia washitakiwa hao wanatakiwa kulipa fidia katika mazingira hayo, hivyo wanaingia katika madeni ili waweze kulipa fidia.

"Ni rai yetu katika utoaji wa adhabu tunaomba uyazingatie utoe adhabu yenye unafuu na inayotekelezeka ili kukidhi haja ya sheria hii ambayo dhamira yake ni kupunguza mrundikano wa mahabusu gerezani. Nimezingatia hoja za pande zote na kwa kuzingatia makubaliano mliyofikia Mahakama inawahukumu kulipa faini ya shilingi milioni moja au kifungo cha miezi sita jela kila mmoja. Washitakiwa wote mlipe fidia ya shilingi bilioni 1.5 kwa Serikali ya Tanzania kwa hasara iliyopatikana,"amefafanua Jaji Banzi.
Katika mashtaka mapya yaliyosomwa na,Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya inadaiwa, washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara.

Imedaiwa Mei Mosi, 2012 na Juni 1, 2015 wakiwa jijini Dar es Salaam, washitakiwa isivyo halali waliandaa ada ya mkopo kwa Serikali ya Tanzania wa dola za Marekani milioni 600, 000,000 kutoka asilimia 1.4 hadi 2.4 na kusababisha Serikali kupata hasara ya dola za Marekani milioni 6,000,00.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news