BODI ya Ligi nchini Tanzania (TPLB) imetangaza ratiba ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2020/2021, Diramakini imekukusanyia..
Ni msimu ambao utashirikisha jumla ya timu 18 huku raundi ya saba vilabu vya Simba na Yanga vikitarajia kukutana Oktoba 18, mwaka huu katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Almas Kasongo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ametangaza ratiba hiyo leo na amesema ligi hiyo itaanza Septemba 6, mwaka huu baada ya mchezo wa ufunguzi wa ligi wa ngao ya jamii kati ya Simba SC dhidi ya Namungo utakaopigwa Agosti 29, mwaka huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Kasongo amesema kuwa, katika upangwaji wa ratiba wamezingatia sana kuendana na kalenda ya CAF pamoja na FIFA.
Mzunguko wa kwanza, pazia litafunguliwa Septemba 6, mwaka huu ambapo Namungo FC watacheza na Coastal Union katika uwanja wa Majaliwa.
Aidha,Biashara United watawaalika Gwambina FC katika Uwanja wa Karume mjini Musoma huku Dodoma Jiji wakirusha karata yao kwa Mwadui FC katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Simba SC ambao ni mabingwa watetezi kwa mujibu wa ratiba hiyo wataanza kuutetea ubingwa wao dhidi ya wageni wa ligi hiyo Ihefu FC ya jijini Mbeya,Mtibwa Sugar watawaalika Ruvu Shooting na Yanga SC wakicheza na Tanzania Prisons .
Pia ratiba inaonyesha kuwa, raundi ya kwanza itakamilika Septemba 7, mwaka huu ambapo KMC wataialika Mbeya City na mwisho Azam FC watacheza na Polisi Tanzania.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo,michezo 306 itapigwa kwenye raundi 34 ambapo ligi hiyo inatarajiwa kumalizika Mei 5, 2021. Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com
Tags
Michezo