MKURUGENZI MTENDAJI WA TIC ATOA WITO KWA WATANZANIA KUYATUNZA MAENEO YA UWEKEZAJI

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimewataka wakazi waishio jirani na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji nchini kutunza maeneo hayo ili yaweze kuchochea uchumi wa Taifa kutokana na uwekezaji unaotarajiwa au uliofanywa kuweza kuimarika.

Wito huo umekuja kufuatia kubainika kwa changamoto ya uchomaji wa mashamba ya jirani na maeneo yalipo mashamba ya Kampuni  ya Uwekezaji ya Aviv ambayo ni kampuni tanzu ya Olam inayojihusisha na uwekezaji wa kilimo cha kahawa, kitendo kinachodaiwa kufanywa na wakazi waishio kwenye maeneo ya jirani.
Makamu Meneja wa Kampuni ya Aviv ambayo ni Kampuni tanzu ya Olam,Steve Kamau (kushoto) akifafanua jambo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt.Maduhu Kazi (mwenye miwani) alipotembelea katika kampuni hiyo Agosti 26,2020 mkoani Ruvuma, Aviv inawekeza katika kilimo cha kahawa mkoani humo.


Katika ziara yake mkoani Ruvuma, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Dkt.Maduhu Kazi alitembelea katika mradi huo mkubwa wa uwekezaji na kuelezwa changamoto hiyo.

“Niwaombe wakazi wanaoishi jirani na maeneo ya uwekezaji, wayatunze maeneo hayo, kwani ni muhimu sana, hii itasaidia kukuza uwekezaji na kuongeza ajira,”alisema Dkt.Kazi. 

Makamu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Aviv, Steve Kamau alisema, licha ya kuwa na uzalishaji mzuri, lakini changamoto hiyo ya uchomaji wa mashamba ya jirani imekuwa ikiwasumbua sana, hata hivyo alikiri kupata ushirikiano toka ngazi ya mkoa kuweza kukabili changamoto hiyo mara inapotokea.

“Sisi tunawekeza kwenye kahawa, sasa hivi tumepanda hekta 2,000 za kahawa aina ya Arabica, tulianza uzalishaji mwaka 2012 hadi 2015, mwaka 2016 tulianza kuvuna. Mwaka huu wa 2020 tumezalisha tani 1,500. Hata hivyo, changamoto ya uchomaji moto mashamba inayofanywa na jirani zetu inaathiri sana kilimo chetu cha kahawa,”alisema Kamau.
 
Kampuni hiyo ya Aviv imekuwa ikishirikiana na jamii katika kuimarisha huduma za jamii ikiwepo ujenzi wa shule na zahanati, huduma za maji safi na salama ambapo kwa mwaka hutumia kiasi cha Dola za Kimarekani zipatazo 12,000 kwa huduma za jamii. Katika uwekezaji huo imetoa ajira za kudumu kwa wakazi 434.

Dkt.Maduhu alitumia fursa hiyo kumuomba mwekezaji huyo kufikiria pia kuwekeza katika usindikaji wa mazao ya chakula, kwa mfano mkoa una ziada ya uzalishaji wa mahindi unaofikia tani 116,660 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kikubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news