Mtendaji Mkuu wa TARURA atoa maagizo kwa Mkandarasi

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi ambaye ni Mbuya’s Contractors Company Limited anayejenga Barabara za Mjini-Matai katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kukamilisha mradi unaotokana na ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli kwa muda kulingana na mkataba, anaripoti Geofrey Kazaula-TARURA...

Amemuelekeza Mkandarasi huyo kuhakikisha anazingatia viwango katika kutekeleza mkataba huo ili barabara ziweze kuwa na ubora unaotakiwa.


Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff (aliyevaa kofia) akiangalia eneo linapojengwa daraja la Kavunja linalounganisha Kata ya Kirando na Korongwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa. (Picha na TARURA).

 
‘‘Unatakiwa kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati, lakini pia unazingatia viwango vinavyotakiwa na mimi mwenyewe nitarudi hapa kujiridhisha,"amesema Mhandisi Seff.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Seff ametembelea miradi ya barabara na madaraja katika halmashauri mbalimbali ndani ya Mkoa wa Rukwa ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi alitembelea miradi ya barabara za lami katika Mji wa Namanyere zilizokamilika na zinazoendelea kujengwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mtendaji Mkuu wa TARURA pia alitembelea na kujionea hali ya Daraja la Kavunja lililopo Kijiji cha Kirando katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa ambapo hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na jinsi ambavyo Ofisi ya Mratibu wa Mkoa wa Rukwa inavyoshughulikia changamoto zilizojitokeza za menejimenti ya mkataba na usanifu wa daraja hilo.

Hivyo, ameahidi kutuma timu ya wataalam kuja kwenye daraja hilo na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kutatua changamoto hizo.

Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff (aliyevaa kofia) akisikiliza maelezo. (Picha na TARURA)


Akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, kiongozi huyo alitembelea na kujionea hali ya daraja la Kankwale lililopo Kata ya Kankwale ambalo pia limeharibika kutokana na mvua nyingi zilizonyesha na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ambapo aliagiza kuwa ujenzi wa daraja hilo uanze mara moja kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ili kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji zinarejeshwa kwa wananchi.

Naye Kaimu Mratibu wa TARURA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Selemani Mziray amesema kuwa katika Mji wa Namanyere, ujenzi wa barabara za lami zinazotokana na Ahadi za Rais, hadi sasa kilomita mbili zimekamilika na kilomita moja ipo katika utekelezaji na itakamilika Agosti 30, mwaka huu.

‘‘Tunajitahidi ili kuhakikisha miradi hii inayotokana na ahadi za Mheshimiwa Rais inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili wananchi waweze kunufaika,”anasema Mhandisi Mziray.


Kabla ya kuhitimisha ziara yake mkoani Rukwa, Mtendaji Mkuu wa TARURA alifanya kikao kazi na mameneja wote wa TARURA waliopo kwenye halmashauri zote zilizopo kwenye Mkoa wa Rukwa ili kutoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujadili namna ya kuendelea kurejesha mawasiliano kwa maeneo yaliyoathiriwa sana na mvua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news