Naibu Waziri Kanyasu aagiza Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori kipewe kitalu cha uwindaji

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii,Constantine Kanyasu ameamuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Dokta Aloyce Nzuki  kutoa  kitalu cha Uwindaji wa Kitalii kwa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka  ili kitumike kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosomea masomo ya Uwindaji Bingwa (Professional Hunters), anaripoti Lusungu Helela kutoka Kilimanjaro. 

Ametoa agizo hilo wakati akizindua Bodi ya Magavana ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilichopo katika Wilaya  ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kanyasu amesema, kitalu hicho cha uwindaji wa kitalii kitakisaidia chuo hicho kuzalisha wataalamu  wenye sifa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Constantine Kanyasu akimkabidhi  begi lenye vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, Profesa Faustine  Bee wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo iliyofanyika katika chuo hicho kilichopo mkoani Kilimanjaro. Picha na WMU/Diramakini.
 
Amesema, kwa sasa Mabingwa wa Uwindaji wa Kitalii wanaofanya kazi hiyo hapa nchini  ni raia wa kigeni na baadhi ya  wazawa waliopo  ni wazee.
 
Amesema, kitalu hicho kitachochea kupata  wataalamu wa kutosha ili kuweza kukabiliana na  uhaba wa wataalamu wa fani hiyo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akimkabidhi begi lenye vitendea kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dokta Aloyce Nzuki  mara baada ya uzinduzi wa Bodi ya Magavana ya Chuo Cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka  iliyofanyika  mkoani Kilimanjaro. Picha na WMU/Diramakini.
 
Kanyasu amesema , chuo hicho kitasaidia  kukabiliana na wafugaji  wanaoingiza vitalu vya uwindaji wa kitalii  kwa vile vitalu vingi  bado vipo wazi hali inayopelekea wafugaji wengi  kuingiza mifugo.
 
Amesema, kitalu hicho hakitasaidia wahitimu pekee kufanya mafunzo kwa vitendo bali  itasaidia wanyamapori kuwa salama kwa sababu chuo hicho kitakuwa na jukumu la kupambana na tatizo la ujangili.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii ,Constantine Kanyasu akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Bodi ya Magavana wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakati wa hafla ya uzinduzi wa hafla hiyo  iliyofanyika chuoni hapo mkoani Kilimanjaro. Picha na WMU/Diramakini.
 
Pia Kanyasu amempongeza Mwenyekiti wa bodi hiyo,  Profesa Faustine Bee kwa kuchaguliwa kwa awamu ya pili ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo pamoja na Magavana wa Bodi kwa asilimia kubwa kuteuliwa tena kuendelea kukitumia chuo hicho. 
 
Awali, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Jaffari Kidegesho amesema , kwa  sasa wanafunzi wa chuo hicho wamekosa maeneo ya kufanyia mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya uwindaji wa kitalii.

Amesema, mwanzo chuo hicho kilikuwa kikiyatumia  mapori ya akiba kwa ajili ya mafunzo hayo ila kwa sasa mapori hayo  yamepandishwa hadhi na kuwa Hifadhi za Taifa hivyo katika hifadhi hizo hakuna shughuli za kibindamu zinazoruhusiwa kufanyika kwa mujibu wa sheria.
 
Naye Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori, Mweka, Profesa Jaffari Kidegesho amesema, kitalu hicho kitasaidia kufanya mafunzo kwa vitendo na hivyo kutasaidia kuwaandaa wahitimu wenye sifa kulingana na mahitaji ya soko.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dokta Aloyce Nzuki amekitaka chuo hicho kuboresha mtaala wa mafunzo hayo ili kuzalisha wataalamu wataoweza kujibu changamoto za soko.
 
 
Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi  ya Magavana wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilichopo mkoani Kilimanjaro  mara baada ya kuzindua Bodi ya Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, wengine ni wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.Picha na WUM/Diramakini. 
 
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaji Rajabu Kundya amesema, suala la uhifadhi na utalii limekuwa na mchango mkubwa sana kwa uchumi wa Taifa hali iliyopelekea Tanzania kuwa na uchumi wa kati.
 
Amesema, shughuli hizo wanazichukulia kwa uzito mkubwa na wanakithamini sana  chuo hicho kwa mchango mkubwa wa kuzalisha wasomi wenye weledi.
 
Itakumbukwa kuwa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka ndio chuo pekee nchini kinachotoa mafunzo ya Uwindaji Bingwa wa Kitalii (PH).
 

  Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news