Ni rasmi Chuo cha Madini kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

* Naibu Waziri Nyongo asema mabadiliko yasiondoe majukumu ya msingi,Profesa Anangisye naye abainisha hakuna hofu chuo kipo mikono salama

IMETHIBITISHWA kuwa sasa Chuo cha Madini kilichokuwa chini ya Wizara ya Madini kitakuwa sehemu ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam,anaripoti Asteria Muhozya na Steven Nyamiti kutoka Nzega.

  1. Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akieleza jambo katika hafla ya kukabidhi Chuo cha Madini (MRI) kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyofanyika Agosti 19, 2020 Kampasi ya Nzega. (Kushoto) ni Prof. WilliamAnangiye Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Madini/Diramakini.

Hayo yalithibitishwa Agosti 19, 2020 wakati wa hafla ya kukabidhi chuo hicho Kampasi ya Dodoma na Nzega kulelewa kwa muda na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam katika hafla iliyofanyika katika Kampasi ya Nzega wilayani Nzega Mkoa wa Tabora.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema  kuwa, tukio hilo ni moja ya hatua za uboreshaji wa Sekta ya Madini pamoja na kuhakikisha nchi ya Tanzania inazalisha wataalam wa kutosha na wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya madini kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Stashahada.

Lengo likiwa ni nchi iweze kusimamia rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia bila kutegemea wataalam kutoka nje.

Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Nzega (kushoto), vongozi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (katikati) na wafanyakazi wa Wizara ya Madini (kulia) wakisikiliza wakati wa hafla ya kukabidhi Chuo cha Madini (MRI) kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika Agosti 19, 2020 Kampasi ya Nzega. Picha na Wizara ya Madini/Diramakini.

Alisisitiza kuwa, Serikali  inaamini kuwa,  ulezi wa Chuo  cha Madini kama ilivyoelezwa kwenye mchakato wa awali, kitaendelea  kutoa mafunzo ya mchundo na mafundi sanifu katika Sekta ya Madini lengo likiwa  kukifanya kitengamae hatimaye kiweze kujiendesha.

"Uleaji utakaotolewa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam ulenge kukiimarisha Chuo cha Madini Kitaaluma, kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi  wa utendaji kazi," alisisitiza Nyongo.


Aliongeza kuwa, mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa na UDSM yasilenge kuondoa majukumu ya msingi ya Chuo cha Madini.

"Ni matarajio ya Serikali na wizara kuwa chuo hiki kitafikia viwango vya kitaaluma vinavyokubaliwa Kitaifa na Kimataifa,"alisema Nyongo.

Akielezea kwamba,  kumekuwepo na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na kutokuwepo kwa sheria ya kuanzishwa Chuo cha Madini, uvamizi  wa maeneo hususan Kampasi ya Nzega na kuongeza kwamba  anaamini  changamoto hizo zitatuliwa chini ya ulezi huo na kwamba hafla hiyo  ni matokeo ya utatuzi wa changamoto hizo.

Pia, alizungumzia  hatua mbalimbali ambazo zimechukukiwa  na Serikali, ambazo zimepelekea Sekta ya Madini sasa imeanza kukua kwa kasi kubwa, ambapo mwaka 2019 iliongoza kwa ukuaji  kwa asilimia 17.7.

Alisema, kutokana na jitihada hizi sasa mapato yanayotokana na madini yameongezeka  ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 zilikusanywa Shilingi Bilioni 346 kutoka Shilingi Bilioni 194  Mwaka 2016/17, kwenye mwaka 2019/2020 zlikusanywa zaidi ya shilingi bilioni 470 ambalo  ndiyo lilikuwa lengo la wizara.

"Malengo kwa mwaka 2020/2021 ni kukusanya shilingi Bilioni 543, tunaweza kufika Bilioni 600, lakini pia tuna ndoto ya kukusanya Shilingi Trilioni Moja kwa mwaka," alisema Naibu Waziri Nyongo.

Aliongeza kuwa,  Rais Dkt. John Magufuli kwa muda mrefu amekuwa akisisitiza kuhakikisha rasilimali zetu ikiwemo madini zinasimamiwa kikamilifu ili ziweze kuwanufaisha watanzania ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchumi hatimaye kupunguza utegemezi.

Aliyataja mafanikio mengine tuliyoyapatikana kwenye Sekta ya Madini kuwa ni pamoja na  kutolewa kwa leseni 221 za uchenjuaji wa Madini, Leseni 4 za uyeyushaji madini (smelting) na Leseni 4 za usafishaji madini (refining).

Pia, alisema wizara imetenga hekta 38.567 kwa ajili ya uchimbaji mdogo na kuwapatia mafunzo wachimbaji wadogo na kuwawezesha kutengeneza maisha yao bila bughudha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu  wa Wilaya  ya Nzega, A. C.P Advera Bulimba  kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora alitoa pongezi kwa Serikali kuchukua hatua za kuboresha chuo hicho na kueleza Serikali ya mkoa na wilaya itashirikiana na chuo kuhakikisha mazingira na mali za chuo zinalindwa.

"Ni matarajio chuo kitaongeza usajili kulingana na mahitaji ya chuo. Tunawahamasisha wazazi walete watoto wao ili kuboresha mkoa wetu,"alisema A.C.P Bulimba.

Aliongeza kwamba,mkoa umefurahia kutokana na hatua hizo zilizochukuliwa kwa   kuwa  zitauwezesha mkoa kupata fursa za kimapato kupitia fursa mbalimbali zitakazotolewa na chuo hicho.

Aidha, aliwasisitiza wazazi mkoani humo kuhakikisha wanapeleka watoto wao ili kupata elimu zinazotolewa na chuo hicho kwa lengo la kuboresha maendeleo ya mkoa huo.

Naye, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa akizungumza katika halfa hiyo alisema kuwa, wazo la Chuo cha Madini kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam lilitoka Wizara ya Madini mwezi Januari, 2018 ambapo uamuzi ulikusudia kukiwezesha Chuo cha Madini kuongeza nafasi za udahili, kuendesha kozi zinazoendana na soko la ajira, kuongeza ufanisi katika maeneo muhimu ya utafiti,uchapishsji na kuongeza huduma zinazotolewa na Chuo cha Madini.

Akielezea uzoefu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam katika kuvilea vyuo vingine alisema kwamba,  uzoefu unaonesha njia ya kulelewa na taasisi kubwa zenye uzoefu ni bora zaidi katika kuziwezesha taasisi changa kujisimamia zenyewe.

  1. Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) waliokaa na wafanyakazi wa Wizara ya Madini kwenye picha ya pamoja na wakati wa hafla ya kukabidhi Chuo cha Madini (MRI) kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika Agosti 19, 2020 katika Kampasi ya Nzega. Picha na Wizara ya Madini/Diramakini.

"Chuo  cha Ardhi-Dar es Salaam ambacho kililelewa na UDSM kuanzia mwaka 1996 mpaka mwaka 2006 kilipoachwa kijiendeshe chenyewe na Chuo Kikuu cha Mzumbe  wakati huo kikijulikana Kama  Insitute of Development Management ( IDM) kililelewa na UDSM kwa kipindi cha muda wa miaka nane na baada ya hapo kiliweza kusimamia na kujiendesha chenyewe na sisi sote ni mashahidi wa mafanikio ya vyuo hivi viwili," alisistiza Mhandisi Mulabwa.

Akielezea kuhusu hatua kadhaa zilizochukuliwa alisema kuwa, katika hatua za kukamilisha mchakato wa kulelewa, Februari 20, 2020 ilisainiwa Hati ya Makubaliano  kati ya Wizara ya Madini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam ambayo iliandaa utaratibu mzima wa kulelewa.

Pia alisema, kutokana na utaratibu uliowekwa katika Hati ya Makubaliano, mambo mbalimbali yalifanyika ikiwemo kutangazwa kwa Order ya kuanzishwa Chuo  cha Madini katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na kuandaliwa kwa muundo wa Taasisi na Muundo wa Utumishi wa Chuo Cha Madini kubainisha mali zilizopo chini ya Chuo Cha Madini.

" Ni matumaini yangu kuwa utoaji wa mafunzo wa Chuo cha Madini utakuwa wa kiwango cha juu, udahili wa wanafunzi utaongezea nchini na kutoka nje ya nchi, miundombinu itaboreshwa na kutimiza jitihada za Serikali za kuhakikisha inakuwa na wataalam wazawa watakaofanya shughuli  mbalimbali katika Sekta ya Madini,"" alisema Mhandisi Mulabwa.

Vilevile alisistiza kuwa, huo kitakapoachiwa kitakuwa na mifumo mizuri ya kujiendesha chenyewe.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Prof. William Anangisye alisema kuwa, Chuo cha Madini kuwa sehemu ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam kinatarajiwa kupata fursa ya kuingia katika wigo mpana zaidi wa kitaaluma.

"Tunafurahi kuwa kwa kupitia mazungumzo ya pamoja kati ya wizara zetu mbili, yaani Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Madini, sasa tumefikia muafaka kuwa Chuo cha Madini Dodoma kitakuwa sehemu ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam baada ya mchakato wake ambao ulianza tangu mwaka 2018,"alisema Prof.Anangisye. 

Aliongeza kwamba, Chuo Kikuu Cha UDSM kimegusa nyanja nyingi za kitaaluma ikiwemo taaluma ya madini , ambapo Idara  ya Jiolojia imetoa wataalam wanaoheshimika duniani na imekuwa na mchango mkubwa sana Kitaifa na kuongeza kwamba, jukumu  hilo la kukilea Chuo Cha Madini linawapeleka Chuo Cha UDSM kuwa karibu zaidi na Watanzania ambalo ndilo lengo la chuo.

Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa (katikati) akizungumza jambo na viongozi mbalimbali katika hafla ya kukabidhi Chuo cha Madini (MRI) kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyofanyika Agosti 19, 2020 katika kampasi ya Nzega.    Kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Prof. William  Anangisye,   na kushoto ni Mhe. A.C.P Advera Bulimba, Mkuu wa Wilaya ya Nzega. Picha na Wizara ya Madini/Diramakini.

" Napenda niwahakikishie Makatibu Wakuu wa Wizara zetu mbili kuwa Chuo Kikuu cha Dar  Es Salaam kina uzoefu mkubwa wa kukuza taaluma baada ya kukabidhiwa vyuo mbalimbali vya Serikali,"alisema Prof.Anangisye.

Prof. Anangisye aliwasisitiza wafanyakazi na watumishi wa Chuo cha Madini kuwa,  wako katika mikono salama na hivyo hawapaswi kuwa na hofu yoyote ya kuwa sehemu ya chuo hicho.

"Masuala yanayohusu mustakabali wa wafanyakazi na wanafunzi, mali za chuo na mengine mengi, yalijadiliwa kwa kina na umakini mkubwa na Kamati Kuu ya kusimamia Ujumuishaji wa Chuo cha Madini Dodoma kwenye Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam. Sisi tunazingatia  yote yaliyopendekezwa na kukubaliwa na tutazingatia wajibu wetu kukiboresha Chuo  cha Madini na kuimarisha viwango vyake vya taaluma,"alisema.

Akizungumzia  nafasi ya  Chuo  Kikuu Cha Dar Es Salaam  katika kuendeleza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli katika kuiendeleza Sekta ya Madini nchini, alisema, moja ya matokeo ya uongozi wake ni kuboresha Sekta ya Madini na kuifanya kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa  nchi yetu, hivyo chuo hicho  kinachukulia  hatua ya kukabidhiwa Chuo cha Madini kama sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kukuza Sekta ya Madini.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu  wa Chuo cha Madini Elvanus Kapira alialeza kwamba Menejimenti ya chuo inaamini kwamba kupitia mpango wa kulelewa, Chuo  cha Madini kitaimarika katika nyanja za kielimu, kitafiti, pamoja na huduma za kutoa  ushauri elekezi huku changamoto zote zinazokikabili chuo ambazo zinapelekea kukua kwa kasi isiyolizisha zitatatuliwa  chini ya mpango wa kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.

Alisema kuwa, menejimenti na wafanyakazi wote wa Chuo cha Madini wanaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote  cha mpango kulelewa ili kufanikisha malengo mahususi ya kuboresha  elimu na huduma zinazotolewa na Chuo cha Madini kwa masilahi mapana ya Taifa letu.

  1. Kamisha wa Madini, Mhandisi David Mulabwa pamoja Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam, Prof. William Anangiye wakikabidhiana nyaraka za kuhitimisha hafla ya kukabidhi Chuo cha Madini (MRI) kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam iliyofanyika Agosti 19,2020  katika Kampasi ya Nzega. Picha na Wizara ya Madini/Diramakini.

"Menejimenti ya Chuo cha Madini inaishukuru Wizara ya Madini kwa jitihada ilizochukua kwa ajili ya kukiendeleza chuo na pia inaishukuru Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kwa kuridhia kukilea chuo hiki,"alisema Kapira.

Pia Kapira akielezea mafunzo yanayotolewa na chuo hicho ni pamoja na mafunzo ya muda mrefu, muda mfupi pamoja na mafunzo maalum kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Chuo cha Madini kilianzishwa mwaka 1982 kwa lengo la kutoa mafunzo ya ufundi sanifu katika Sekta ya Madini. 

Chimbuko la kuanzishwa kwake  ni uhitaji uliokuwepo wa wataalm wa kada za ufundi katika miradi ya  utafiti, wa maji, madini ya bati na metali nyingine uliojulikana Kama Mineral and Ground Water Exploration Project (MGWEP) mkoani Kagera.

Karibu! Tovuti hii ya www.diramakini.co.tz imesajiliwa rasmi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupewa leseni namba TCRA/OCS-BL/0197/2020 chini ya Diramakini Business Limited iliyosajiliwa nchini Tanzania kwa ajili ya kukuhabarisha, kukuelimisha na kukupasha habari mbalimbali toka ndani na nje ya nchi. Je? Una habari,maulizo au tangazo, unataka kutupa ufadhili? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com Asante.

 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news