MKUU wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Geita kuita kampuni zote zinazofanya kazi ndani ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) na kuzielekeza kukarabati shule mbalimbali za msingi na sekondari katika Halmashauri ya mji wa Geita, anaripoti Robert Kalokola kutoka Geita.
Mhandisi Gabriel ametoa agizo hilo wakati akipokea
madarasa matano na ofisi moja ya walimu ambavyo vimekarabatiwa na
kampuni ya uchimbaji wa madini chini kwa chini ya African Underground
Mining Services (AUMS).
Amesema kuwa, kampuni hiyo ya AUMS kama imeweza kutenga
bajeti na kukarabati madarasa hayo hata makampuni mengine hayawezi
kushindwa kukarabati shule zilizosalia.
Pia amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Geita, Fadhili Juma kukaa pamoja na kampuni hizo na
kuzielekeza kufanya ukaratabati huo ikiwa ni sehemu ya makampuni hayo
kuhudumia jamii (CSR).
Naye Mkurugenzi
wa Kampuni ya African Underground Mining Services, Tom Sawyer amesema
kuwa, kampuni hiyo itaendelea kusaidia Serikali kutimiza malengo yake
katika maendeleo ya wananchi.
Mkurugenzi wa kampuni ya
AUMS Tom Sawyer akizungumza wakati anakabidhi vyumba 5 na ofisi moja ya
walimu kwa mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel. Picha na Robert Kakokola. |
Amesema kuwa, kampuni hiyo itajenga vyoo vya kisasa katika shule hiyo hiyo ya Nyanza kwa ajili ya wasichana.
Sawyer ameongeza
kuwa, kampuni imeamua kuwekeza katika elimu kwa sababu elimu inasaidia
mtoto na jamii nzima na kampuni yake inatamani kuajiri vijana watakaosoma na kuhitimu kutoka shule hiyo ya Nyanza.
Kwa upande wake Mkuu
wa Shule ya Nyanza, Kassim Clifford amesema kuwa, kampuni hiyo ilitoa
sh.milioni 50 kwa ajili ya kukarabati vyumba hivyo vitano vya madarasa na
ofisi moja ya walimu.
Ameongeza
kuwa, ukarabati huo umetumia jumla ya sh.milioni 61.2 ambazo
zilitolewa na Kampuni hiyo ya AUMS na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji
wa Geita.
Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com
Tags
Habari