BAADHI ya
watendaji wa wilaya na halmashauri za mikoa ya Kanda ya Kati
inayojumuisha mikoa ya Iringa, Dodoma na Singida wameipongeza Serikali
kwa kutunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, kwa lengo la
kuviendeleza na kuvimarisha vikundi vyote vinavyofanya biashara ya
huduma ndogo za fedha na kutoa mafunzo ya kuwawezesha wananchi
kutekeleza sheria hiyo, anaripoti Farida Ramadhani kutoka Morogoro.
Hayo yameelezwa mjini Morogoro katika mafunzo ya Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kwa watendaji hao ambayo yameandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (FSDT).
Watendaji hao wameahidi kuisaidia Serikali kusimamia na kuhamasisha zoezi la usajili na ukataji leseni kwa watoa huduma ndogo za fedha kwa mujibu wa sheria ili kuwezesha utekelezaji wa sheria hiyo kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.
Wakitoa maoni yao kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo watendaji hao wamesema kuwa, elimu hiyo imetolewa wakati mwafaka na wanaamini itakuwa mwarobaini wa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili sekta ndogo ya fedha ikiwemo utoaji wa mikopo kwa wananchi kwa vigezo na masharti magumu yanayowasababishia wananchi madhara mbalimbali kama vile kufilisiwa.
“Wananchi hususan wastaafu wameteseka kwa muda mrefu kutokana na mikopo ambayo masharti yake hayapo wazi, unakuta mstaafu anakopa fedha ndogo, lakini baada ya miezi michache anatakiwa kulipa mara kumi ya kile alichokopo hadi unashangaa huyu mtu wamemkata riba kwa asilimia ngapi na wakopeshaji ukiwauliza mikataba wanakuwa sio wawazi,”anasema Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida,Sango Songoma.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa,Sara Komba ameshauri elimu hiyo itolewe kwa kasi ili wananchi wengi hususan wale wa vijijini waweze kupata elimu hiyo ambayo itawanusuru na matapeli wanaoitumia vibaya Sekta Ndogo ya Fedha na kuwaongezea wananchi umaskini.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja ambaye aliwataka watendaji hao kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha sheria inatekelezwa ili kuboresha usimamizi na udhibiti wa sekta ndogo ya fedha nchini na kuwa na sekta ya fedha iliyo endelevu na yenye kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Ameahidi kuwa elimu hiyo itaendelea kutolewa nchi nzima ili kuhakikisha wadau wote muhimu wanafikiwa na kuwawezesha kufuata matakwa yote ya Sheria kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.
e, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com