Mpira umemalizika hapa viwanja vya Sheikh Amri Abeid, Arusha kwa Simba kuibuka kidedea.
Simba SC 2-0 vs Namungo FC, wafungaji ni Boko na Bernald Morison. Huku Jonas Mkude akiibuka mchezaji bora. Kutoka hapa Arusha Crew ya www.diramakini.co.tz haina la ziada.
Simba SC wamefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii 2020 baaa ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Mchezaji mpya, winga Mghana Bernard Morrison ndiye nyota wa mchezo huo baada ya kuliandaa bao la kwanza kipindi cha kwanza na kufunga la pili kipindi cha pili.
John Raphael Bocco, nahodha wa Wekundu hao aliifungia Simba SC bao la kwanza kwa penalti dakika ya saba.
Ni baada ya Morrison kuangushwa kwenye boksi kabla ya winga huyo Mghana kufunga la pili dakika ya 60 akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama.
Huu unakuwa ushindi wa sita wa Ngao ya Jamii kwa Simba SC tangu ianzishwe mwaka 2001, na kuwa timu iliyobeba taji hilo mara nyingi zaidi, ikifuatiwa na watani wa jadi, Yanga SC waliotwaa mara tano ngao hiyo.
Simba SC imebeba Ngao ya Jamii katika miaka ya 2011 ikiifunga Yanga 2-0, 2012 ikiifunga Azam FC 3-2, mwaka 2017 ikiwafunga Yanga kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 0-0, 2018 ikiwafunga Mtibwa Sugar 2-1, mwaka 2019 ikiwafunga Azam FC 4-2 na leo.
Aidha,Yanga SC ilikuwa washindi wa kwanza wa Ngao ya Jamii mwaka 2001, wakati huo ikiitwa Ngao ya Hisani baada ya kuwafunga Simba 2-1, kabla ya kubeba tena 2010 wakiwafunga tena Simba kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya 0-0, 2013 wakaichapa Azam FC 1-0, 2014 wakiitandika Azam FC 3-0 na 2015 wakiifunga Azam FC kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0.
Timu nyingine zilizotwaa Ngao ya Jamii ni Mtibwa Sugar mwaka 2009 wakiifunga Yanga SC 1-0 na Azam FC 2016 wakiifunga Yanga pia kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2.