TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Manyara imemfikisha mahakamani Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Magugu, Adeltus Richard Rweyendera kwa tuhuma za rushwa, inaripoti Diramakini..
Hakimu huyo anatuhumiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 150,000 kutoka kwa wanafamilia mjini humo.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Isdory Kyando amesema, mtuhumiwa huyo alipokea rushwa hiyo kutoka kwa wazazi na ndugu wa washtakiwa wanne ambao walikuwa wanashtakiwa kwenye kesi namba 242/2020 ikiwa ni kishawishi cha kuwasaidia na kuwaachia washtakiwa hao kwenye kesi tajwa ambayo alikuwa anaisikiliza.
Amesema, awali TAKUKURU Mkoa wa Manyara ilipokea taarifa kutoka kwa wasiri ikifafanua kuwa Hakimu aliomba kiasi hicho cha fedha akiwataka wazazi na ndugu wa washtakiwa hao wachangishane.
Kaimu Mkuu huyo amesema kuwa, baada ya kupokea taarifa hiyo, TAKUKURU walifanya uchunguzi wa kina na kubaini ni kweli kesi tajwa ilikuwepo katika Mahakama ya Mwanzo Magugu na kwamba kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Adeltus Richard Rweyendera huku kesi hiyo ikitajwa mara kadhaa bila kusikilizwa tangu ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza Agosti 3, mwaka huu.
Amesema, uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa, wananchi hao walikamatwa kwa tuhuma za uzururaji, miongoni mwao wakiwa kwenye maeneo yao ya biashara.
Aidha, TAKUKURU walibaini kuwa hakimu huyo aliwataka washtakiwa wote wanne wachange kiasi hicho cha fedha.
Kyando amesema, baada ya kujiridhisha na ukweli huo maafisa wa taasisi hiyo, waliandaa mtego wa rushwa na kufanikiwa kumkamata hakimu akiwa amepokea kiasi cha shilingi 150,000 fedha ambazo aliziweka kwenye droo ya meza yake mara baada ya kuzipokea.
Pia TAKUKURU imemuunganisha kwenye mashtaka, Issaya Kiluma ambaye alikubaliana hakimu huyo kutoa rushwa hiyo akichangia jumla ya shilingi 40,000 ikiwa ni sehemu ya shilingi 150,000ambazo hakimu alikamatwa nazo.
Kyando ameongeza kuwa,Kiluma alikuwa miongoni mwa ndugu wa washtakiwa ambaye alikubaliana na hakimu kutoa kiasi hicho cha fedha pasipo kutoa taarifa TAKUKURU.
Amesema kuwa, mwananchi huyo ataunganishwa kwenye mashtaka ya kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kutoa rushwa ambapo kosa hilo lina uzito sawa na kosa la kupokea rushwa.
Wakati huo huo, TAKUKURU imetoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na Watanzania kwa ujumla kuacha kuwashawishi na kutoa rushwa kwa watumishi wa Idara ya Mahakama na kwingineko kokote na pale wanapoombwa rushwa wasisite kutoa taarifa katika ofisi za TAKUKURU zilizopo kote nchini.
Pia Kyando, amewataka watumishi wa idara ya mahakama ambayo ni wadau wakubwa wa mapambano dhidi ya ya rushwa na ambao wanafanya kazi muhimu sana ya kusimamia haki za watanzania kuhakikisha kuwa wanawasimamia ipasavyo watumishi wachache ambao sio waadilifu na kuwachukulia hatua stahiki pale inapothibitika kuwa wamejihusisha na vitendo hivyo.
Karibu! Tovuti hii ya www.diramakini.co.tz imesajiliwa rasmi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupewa leseni namba TCRA/OCS-BL/0197/2020 chini ya Diramakini Business Limited iliyosajiliwa nchini Tanzania kwa ajili ya kukuhabarisha, kukuelimisha na kukupasha habari mbalimbali toka ndani na nje ya nchi. Je? Una habari,maulizo au tangazo, unataka kutupa ufadhili? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com Asante.