HASSAN NASSOR MOYO ambaye ni mwanasiasa mkongwe na muasisi wa Mapinduzi Zanzibar amefariki usiku wa kuamkia leo, Agosti 18, 2020, nyumbani kwake mkoani Tanga.
Moyo alikuwa mwanachama wa Chama cha Afro Shirazi (ASP) tangu kilipoanzishwa Februari 5, 1957 baadaye Februari 5, 1977 akajiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa na kadi namba 7.
Aidha ndiye alikuwa Mratibu Mkuu wa Maridhiano ya Zanzibar ya Novemba 5, 2009 yaliyowakutanisha Rais Mstaafu wa Zanzibar (awamu ya sita), Dk Aman Abeid Karume na Maaalim Seif Sharif Hamad katika kutafuta mbinu ya kuondoa tofauti iliyokuwepo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010.
Aprili 19, 2015, Moyo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar, alivuliwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi CCM, hatua iliyofikiwa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Magharibi, Unguja Viswani Zanzibar.