TBS yateketeza vyakula, vipodozi vilivyoisha muda wa matumizi, kupigwa marufuku nchini Tanzania

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza jumla ya tani 2.2 za bidhaa zilizoisha muda wake na zilizokatazwa kutumika zenye thamani ya shilingi 20,150,000, anaripoti  Jacquiline Mrisho  kutoka MAELEZO.

Takwimu hizo zimetolewa jijini Dodoma na Afisa Mdhibiti Ubora wa shirika hilo Kanda ya Kati, Sileja Rushibika wakati alipokuwa akisimamia zoezi la uteketezaji wa bidhaa hizo.

Rushibika amesema kuwa, zoezi la kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia sokoni vikiwemo vyakula na vipodozi ni jukumu la kawaida na lipo kwa mujibu wa Sheria ya Viwango na Sheria ya Fedha.                                                                                                                                                      

Afisa Mdhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati, Sileja Rushibika akisaidia kukusanya bidhaa ambazo zimeisha muda wa matumizi na zilizokatazwa kutumika zikiwa tayari kwa kuteketezwa katika dampo la Chidaya lililopo jijini Dodoma. Picha na MAELEZO/Diramakini.

 “Leo tumeteketeza jumla ya tani 2.2 ambapo kati ya bidhaa hizo, kilo 1200 ni vyakula vilivyomaliza muda wake ambavyo thamani yake ni shilingi milioni 6, kilo 820 ni vipodozi vilivyoisha muda wake vyenye thamani ya shilingi milioni 10 pamoja na kilo 180 za vipodozi vilivyokatazwa vyenye thamani ya shilingi 4,150,000,”amesema Rushibika.

Rushibika ametoa rai kwa wafanyabiashara ambao sio waaminifu wanaouza bidhaa zilizokataliwa au kuisha muda wake kuacha tabia hiyo na badala yake wazitenge na kufuata utaratibu wa shirika hilo wa kuziteketeza.

Afisa Mdhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati, Sileja Rushibika (kushoto) na Afisa Usalama wa Chakula wa shirika hilo Kanda ya Kati, Vicent Meleo (kulia) wakikagua baadhi ya bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zilizokatazwa kutumika kabla ya kuteketezwa katika dampo la Chidaya jijini Dodoma. Picha na MAELEZO/Diramakini.

Aidha, wananchi wanatakiwa kuwa na jadi ya kusoma muda wa matumizi ya bidhaa kabla hawajanunua kwa sababu bidhaa zote zimeandikwa.

Amesisitiza kuwa, suala la kudhibiti ubora sio la TBS pekee bali wananchi wanaweza wakashiriki hata kwa kutoa taarifa ili shirika liweze kufuatilia hali itakayopunguza gharama zisizo za lazima kwa Serikali.  

Burudoza likiendelea na kazi ya kuteketeza bidhaa zilizoisha muda wake na zilizokatazwa kutumika baada ya kukamatwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Picha na MAELEZO/Diramakini.

Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula wa TBS Kanda ya Kati, Vicent Meleo, amewasisitiza wananchi kuacha matumizi ya vipodozi vilivyokataliwa kwa sababu vinaharibu ngozi zao na kusababisha saratani, amewataka pia kutotumia dawa kama vipodozi na badala yake wafuate ushauri wa wataalam wa afya.

Zoezi la ukaguzi wa bidhaa hizo ni endelevu, zoezi hilo limefanyika katika mikoa ya Singida, Tabora na Dodoma. 

Karibu! Tovuti hii ya www.diramakini.co.tz imesajiliwa rasmi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupewa leseni namba TCRA/OCS-BL/0197/2020 chini ya Diramakini Business Limited iliyosajiliwa nchini Tanzania kwa ajili ya kukuhabarisha, kukuelimisha na kukupasha habari mbalimbali toka ndani na nje ya nchi. Je? Una habari,maulizo au tangazo, unataka kutupa ufadhili? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com Asante.

 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news