VIONGOZI wa dini wamewaasa wananchi kuepuka kutumiwa na wanasiasa wasiolitakia mema Taifa huku wakiweka mbele maslahi yao, anaripoti mwandishi wetu kutoka Dodoma.
Askofu Mstaafu wa Kanisa la EAGT, Askofu Evance Chande amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza katika mkutano maalum wa viongozi wa dini.
Chande amesema kuwa, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwatumia wananchi vibaya kwa maslahi yao, hivyo kuwataka wananchi kuwaepuka na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
“Kuelekea Uchaguzi Mkuu niwaase watanzania wote kuzingatia ulinzi wa amani iliyopo na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kuchochewa na baadhi ya viongozi wa siasa, kama viongozi wa dini lazima tuseme ukweli na isitafsiriwe kwamba tunatumiwa na chama chochote cha siasa,"amesisitiza Askofu Chande.
Amesema kuwa, viongozi wa dini kazi yao ni kueleza ukweli ili wananchi wafanye uamuzi sahihi na wenye maslahi ya Taifa na sio watu wachache kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa ya kuleta mageuzi ya kweli kwa wananchi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo inayoteklezwa.
Aliongeza kuwa Serikali iliyopo madarakani kwa sasa imefanikiwa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na inaendelea kuchukua hatua.
Akizungumzia umuhimu wa amani Askofu Chande amesema kuwa lazima kila mtanzania aone umuhimu wa kutunza amani kwa kuangalia mifano ya nchi jirani zilizoshindwa kutunza amani na matokea yake wahanga wakuu ni wanawake na watoto amani inapotoweka.
Kwa upande wake Shehe Abdallah Msafiri amesema, watanzania hawana budi kuungana pamoja na kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ameliwezesha Taifa kuvuka salama katika janga la Corona kwa kuwa alimtanguliza Mungu na amekuwa akionesha kumtegemea Mungu katika kila jambo.
“Dini ni muhimu na ni msingi wa kujenga amani, umoja na mshikamano kwa wananchi wote hivyo viongozi wanalo jukumu kubwa la kuendelea kuhakikisha kuwa amani iliyopo inalindwa na kudumishwa kwa maslahi ya Taifa,"amesisitiza Shehe Msafiri.
Akifafanua amesema kuwa kiongozi bora ni yule anayemtanguliza Mungu kama anavyofanya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa ameiwezesha nchi kufikia maendeleo ya kweli.
Naye Katibu wa Dawati la Jinsia, Wanawake wa Madhehebu ya Dini,Zainabu Juma Ally amesema kuwa , wanawake wanajivunia kuwa na Rais mcha Mungu na anayewajali na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuwaasa wanawake kuepuka kutumiwa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020.
“Tunaishukuru Serikali yetu kwa kuendelea kutekeleza miradi inayolenga kuwawezesha wananchi hasa kinamama katika maeneo yetu hasa kwa sasa ambapo wanawake wengi wamejikomboa kiuchumi," amesisitiza Zainabu.
Viongozi wa dini kutoka dini na madhehebu mbalimbali wamekutana jijini Dodoma kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2020.
Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com