NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dokta Angeline Mabula
ametoa hati 315 kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya
Ilemela ikiwa ni juhudi zake za kuhakikisha walimu wa manispaa hiyo
wanamilikishwa ardhi kwa gharama nafuu, anaripoti Munir Shemweta, WANMM...
Walimu waliopatiwa hati za viwanja ni sehemu ya walimu 525 walioomba kupatiwa
viwanja katika eneo la Nyamiswi Manispaa ya Ilemela ambapo wengine walishindwa
kukamilisha malipo ya viwanja hivyo.
Akizungumza wakati wa kugawa hati hizo kwa walimu wa shule za msingi na
sekondari za Manispaa ya Ilemela, Dokta Mabula mbali na kuwapongeza walimu hao kwa
kukamilisha malipo hadi kumilikishwa ardhi na kuwataka kuzitumia hati
hizo kwa shughuli za maendeleo.
Aidha, Dokta Mabula ambaye ndiye aliyewahamasisha walimu hao kujiunga pamoja kwa
ajili ya kupata viwanja aliyataka makundi mengine maalum kujiunga pamoja kwa
lengo la kuona namna ya kuyasaidia kupata viwanja katika Halmashauri ya
Manispaa ya Ilemela.
"Suala la makazi siyo la walimu pekee, tuone kama kuna kundi lingine maalum
nalo likajiunga kama walivyojiunga walimu na kuchangia fedha ili kupatiwa
viwanja,"amesema Naibu Waziri Mabula.
Kwa mujibu wa Dokta Mabula kilichofanyika kwa walimu wa Manispaa ya Ilemela ni
juhudi za Rais Dokta John Pombe Magufuli kutaka kila mwenye ardhi awe na umiliki ili
kujua mipaka yake na kupata hati kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi na
wakati huo kuitumia hati kwa shughuli za maendeleo.
Amewaasa walimu kutumia benki ikiwemo Benki ya NMB kuomba mikopo ya ujenzi wa
nyumba ili kuwezesha eneo walilopata kwenda kwa kasi hasa ikizingatiwa eneo
hilo limepakana na eneo la Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo cha Afya na Hospitali ya
Wilaya ya Ilemela na kubainisha kuwa eneo hilo ni zuri na hata kama walimu hao
hawatakaa wanaweza kupangisha na kuingiza fedha kidogo kidogo.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya mradi wa viwanja vya walimu katika
halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Albert Mahuyu amesema pamoja na kamati yake
kukutana na changamoto kadhaa wakati wa zoezi hilo ikiwemo baadhi ya walimu
kushindwa kukamilisha malipo kwa wakati, lakini imefanikisha upimaji viwanja 525
na kuingiza kiasi cha shilingi milioni 404.
Sehemu ya walimu wa Manispaa ya Ilemela waliopatiwa hati
na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dokta Angeline Mabula
wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Mwanza. (Picha na Munir Shemweta). |
Naye Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa Baraka Ladislaus amesema, benki yake iko tayari kutoa mikopo kwa walimu na kubainisha mikopo inayotolewa na benki hiyo kuwa ni ile ya kununua, kuezeka na kumalizia nyumba pamoja na mkopo wa kurudishiwa fedha uliyojengea nyumba na mikopo iko hadi ya milioni 200 na unarejesha kidogokidogo kwa takribani miaka mitano.