TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetakiwa kuhakikisha wananchi wanapata haki wanazostahili popote pale wanapoenda kupata huduma nchini, iwe ni kwenye taasisi za umma au binafsi, anaripoti James K.Mwamyoto kutoka Namtumbo.
Agizo hilo limetolewa wilayani Namtumbo jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni Mstaafu George Huruma Mkuchika wakati akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mheshimiwa Mkuchika amefafanua kuwa, TAKUKURU inatakiwa kuwajengea wananchi imani ya kiutendaji ili pale inapotokea wananyang’anywa haki zao na mtu au taasisi yoyote kwa njia za rushwa, TAKUKURU ndio iwe ni kimbilio lao huku wakiwa na imani kuwa watasaidiwa ipasavyo na taasisi hiyo.
“Nawasihi, endeleeni kuwang’ata wala rushwa na mafisadi wote ili mradi msimuonee au kumpendelea yeyote, na endeleeni kuifanya haki ndio nguzo ya utendaji kazi wenu wa kila siku,” Mheshimiwa Mkuchika alihimiza.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja akitoa maelezo kuhusu jengo hilo alisema, uzinduzi wa jengo la TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo ni ushaidi tosha kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Joseph Magufuli imeonesha nia na dhamira ya dhati ya kukabiliana na vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma nchini.Bibi Seja, amemtibitishia Mheshimiwa Mkuchika kuwa, Watumishi wa TAKUKURU wilayani Namtumbo watatumia jengo la ofisi hiyo kuhakikisha wanapambana na vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhirifu kwa manufaa ya wananchi na maslahi ya taifa.
Mheshimiwa Mkuchika amezindua jengo hilo la TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli ambaye tangu aingie madarakani amefanya kazi kubwa ya kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini.
Karibu! Tovuti hii ya www.diramakini.co.tz imesajiliwa rasmi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupewa leseni namba TCRA/OCS-BL/0197/2020 chini ya Diramakini Business Limited iliyosajiliwa nchini Tanzania kwa ajili ya kukuhabarisha, kukuelimisha na kukupasha habari mbalimbali toka ndani na nje ya nchi. Je? Una habari,maulizo au tangazo, unataka kutupa ufadhili? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com Asante.