WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewataka wananchi wa Kijiji cha
Kidoka wilayani Chemba mkoani Dodoma kutoa taarifa kwa wakati zinazohusu
migogoro ya wakulima na wafugaji ili wizara yake iweze kuifanyia kazi, anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Chemba.
Mpina ameyasema hayo alipotembelea kijiji hicho akiwa na lengo la kusikiliza changamoto za wafugaji ili ziweze kufanyiwa kazi ambapo
changamoto nyingi zilizotajwa na wafugaji hao zinahusisha wizara
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Nishati,Ardhi na Kilimo, Mifugo
na Uvuvi.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akilakiwa wakati alipowasili wilayani
Chemba leo kusikiliza changamoto zinazowakabili wafugaji. Picha na WMU/Diramakini. |
Akianisha changamoto hizo, mwananchi mfugaji wa kijiji hicho, Abuu Mikidadi amesema, kijiji hicho kinakabiliana na changamoto ya eneo la malisho ya mifugo,ambapo kulikuwa na eneo la wazi lilitengwa kwa ajili ya malisho, lakini limevamiwa na wakulima ambapo wafugaji wakiingiza mifugo yao wanavamiwa na kupigwa. Amesema, pia kuna changamoto ya josho la kuogeshea mifugo ya pamoja na pembejeo za mifugo.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mpina amesema, Serikali ni moja na
inafanya kazi kwa kushirikiana,hivyo hawezi kuyakimbia matatizo hayo na
atahakikisha anafikisha ujumbe kwa wizara nyingine.
“Tunayo kazi ya kufanya kama Serikali kuangalia namna gani changamoto hizi zinaweza kutatuliwa kama vile kupunguza gharama za umeme kwa kuzungumza na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuweza kushusha tozo ili wakulima na wafugaji kijijini hapo waweze kufanya kazi bila gharama yoyote na Serikali imepunguza tozo za kuogeshea mifugo na italeta pembejeo za mifugo na kuuzwa kwa bei elekezi,” amesisitiza.
“Kuna haja ya kukaa na Waziri wa Kilimo, kuangalia huu Mradi wa Umwagiliaji Chemba unaolalamikiwa na wakulima na wafugaji unawezaje kuboreshwa ili wananchi wapate faida,"ameongeza.
Mpina ameshauri viongozi wa Serikali ya kijiji na Serikali ya wilaya wakae ili waweze kupata suluhisho.
“Nitaleta timu inayoshugulikia migogoro toka wizarani kwangu pamoja na wataalam waje hapa kutafuta majawabu yasiyo na upendeleo, asidhulumiwe mtu yoyote asinyanyaswe mtu yeyote, kila mtu apate haki yake na wataleta mapendekezo serikalini,"amebainisha Waziri huyo.
Mpina amesema kuwa,hakuna mfugaji anayeruhusiwa kuingiza mifugo kwenye mashamba ya watu
wengine, na kuwataka wananchi watoe taarifa kwa wakati kwa wataalam wa
kilimo na mifugo na kwa Jeshi la Polisi.
Wananchi wa Kijiji cha Kidoka ambao ni wakulima na wafugaji wakimsikiliza Waziri
Mpina (hayupo pichani) baada ya kuwasilisha changamoto zao. Picha na WMU/Diramakini. |
“Hatuwezi kuwa na mfugaji anayedharau shughuli za wengine na hakuna anayeweza kuishinda Serikali,"amesema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Dkt.
Semistatus Mashimba amesema, kufuatia changamoto ya matumizi makubwa ya
umeme wananchi waliomba Serikali kwa kupitia TANESCO kuwaunganisha na umeme wa sola ambapo mapendekezo hayo
yanafanyiwa kazi yakienda sambamba na kuangalia uwezekano wa wananchi
hao kuhamishiwa katika tozo ndogo ili waweze kumudu gharama.
Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com