JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza nafasi za kujiunga na mafunzo ya jeshi hilo kwa kujitolea kwa mwaka 2020, anaripoti Frank Mvungi kutoka MAELEZO.
Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi hilo, Kanali Julius Kadawi ameyabainisha hayo jijini Dodoma katika makao makuu ya jeshi hilo yaliyopo mjini Chamwino jijini Dodoma.
Amesema kuwa, Mkuu wa Jeshi hilo Meja Jenerali Charles Mbuge
anawatangazia vijana wote wa Tanzania Bara na Visiwani nafasi za
kujiunga na mafunzo hayo ili waweze kujengewa stadi za kuweza kujiajiri
na kuwa wazalendo.
“Jeshi
la Kujenga Taifa linapenda kuwaarifu vijana watakaopata fursa hiyo kuwa
halitoi ajira kwa vijana, pia halihusiki kuwatafutia vijana ajira
katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama na mashirika mbalimbali ya
Serikali na yasiyo ya Kiserikali,"amesisitiza Kanali Kadawi.
Ameongeza
kuwa, uratibu wa vijana kuomba na hatimaye kuchaguliwa kujiunga na
mafunzo hayo, unaratibiwa na ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya ambako
mwombaji anaishi.
Akifafanua
amesema kuwa, jeshi hilo linatoa mafunzo ambayo yatawasaidia vijana
kujiajiri wenyewe mara baada ya kumaliza mkataba wao na JKT.
 |
Mkuu wa Tawi la
Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kanali Julius Kadawi akisisitiza
kuhusu nafasi zilizotolewa kwa vijana wanaopenda kujiunga na Jeshi hilo
kwa kujitolea kwa mwaka 2020, hayo yelijiri Agosti 20, 2020 Makao
Makuu ya jeshi hilo Chamwino mkoani Dodoma.
(Picha na MAELEZO/Diramakini).
|
“Kutokana
na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID- 19), tahadhari za kuzuia
maambukizi ya ugonjwa huo kama zilivyoelekezwa na Serikali kupitia
Wizara ya Afya zitazingatiwa kwa kipindi chote vijana watakapokuwa
katika mafunzo,”amesisitiza Kanali Kadawi.
Aidha, amebainisha kuwa
Meja Jenerali Charles Mbuge anawaalika vijana wote watakaopata fursa
hiyo kwenda kujifunza uzalendo, ukakamavu, stadi za kazi, stadi za
maisha na pia kuwa tayari kulilinda na kulitumikia Taifa.
Baadhi
ya sifa za vijana wanaotakiwa ni pamoja na; kuwa raia wa Tanzania, awe
na afya njema, mwenye nidhamu na tabia nzuri na hajawahi kupatikana na
hatia Mahakamani na hajawahi kufungwa, asiwe ametumikia Jeshi la
Magereza, Polisi, KMKM, Chuo cha Mafunzo, wala kuajiriwa na idara
nyingine serikalini.
Kigezo kingine asiwe amepitia JKT katika operesheni za nyuma, asiwe amejihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.
Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) limekuwa likiwaandaa vijana kujiajiri kwa
kuwajengea stadi za maisha na kuwawezesha kuwa wazalendo, waadilifu na
walio tayari kulilinda Taifa.
Karibu! Tovuti hii ya www.diramakini.co.tz imesajiliwa
rasmi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupewa leseni namba
TCRA/OCS-BL/0197/2020 chini ya Diramakini Business Limited iliyosajiliwa nchini
Tanzania kwa ajili ya kukuhabarisha, kukuelimisha na kukupasha habari
mbalimbali toka ndani na nje ya nchi. Je? Una habari,maulizo au tangazo,
unataka kutupa ufadhili? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com Asante.