Wewe ni mchimbaji mdogo? NMB wanakuita unufaike na sehemu ya Bilioni 32/- walizowatengea

BENKI ya NMB Plc imetenga shilingi Bilioni 32 kwa ajili ya mikopo kwa wachimbaji wadogo nchini, Diramakini inakujuza kwa kina..

Mkuu wa Idara ya Biashara wa benki hiyo, Alex Mgeni ameyasema hayo wakati wa Kongamano la Wafanyabiashara (NMB Business Club) jijini Mwanza.

 Amesema, kutolewa kwa mikopo hiyo ni matokeo ya maboresho ya sheria na sera kwenye sekta ya madini yanayofanywa na Serikali kwa lengo la kuongeza tija.

 “Mikopo hiyo ambayo imeanza kutolewa tangu Januari, mwaka huu inahusisha gharama za kununua vifaa vya uchimbaji ikiwemo mitambo na magari ya kubebea mchanga wa madini migodini,”amesema Alex.

Kuhusu madhara ya janga la corona kwa sekta ya biashara, Mgeni alipongeza juhudi za Serikali zilizofanikisha kutokomezwa kwa ugonjwa huo uliosababisha changamoto katika mfumo wa biashara na uwekezaji. 

Amesema, kutokana na mifumo ya biashara kupata changamoto, NMB iliwasaidia wateja wake ambao biashara zao ziliathirika zaidi, hasa wale wa sekta ya utalii.

Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB, Alex Mgeni akizungumza kwenye Kongamano la Biashara (NMB Business Club) jijini Mwanza lililoratibiwa kwa ajili ya kuwapa elimu wafanyabiashara zaidi ya 200 kuhusu huduma za kifedha na faida za kutumia huduma za benki hiyo.

“Kila mfanyabiashara aliyepata changamoto na kutifikia tulizungumza naye kutafuta namna ya kumsaidia. Wapo waliopunguziwa viwango vya marejesho na wengine marejesho yao yalisimamishwa kwa muda, hasa wale wa sekta ya utalii walioathirika zaidi,”amesema.

Akizungumzia NMB Business Club, Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus amesema, kongamano hilo linatoa fursa kwa benki kusikiliza, kupokea na kufanyia kazi hoja za wateja.

“Kupitia hoja na mrejesho kutoka kwa wateja wetu wakiwemo wafanyabiashara, NMB tunapata fursa ya kuboresha huduma na bidhaa zetu,”amesema Ladislaus

Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus akipata maelezo kutoka kwa msindika mvinyo,Rose Stephen, kwenye kongamano la wafanyabiashara jijini Mwanza. 

Mfanyabiashara, Contilda Magweti wa jijini Mwanza amesema, licha ya kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara, kongamano hilo la kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini pia huwapa fursa ya kukutana na kujadiliana uso kwa uso na viongozi na watendaji wa benki.

“Kwa kukutana pamoja tunapata fursa ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu kibiashara, NMB iangalie uwezekano wa kongamano hili kufanyika angalau mara mbili kwa mwaka,”amesema Magweti.

Aliwashauri wafanyabiashara na wajasiriamali wenzake kuendelea kusaidiana maarifa ya kutafuta masoko ya bidhaa zao kwa pamoja.

 

  Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news