SHIRIKA lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania limetumia zaidi ya shilingi bilioni 12 kwa miaka 17 kuendesha miradi mbalimbali katika mradi wao mkuu uliojulikana kama Katerero AP Halmashauri ya Wilaya Bukoba mkoani Kagera na kuwanufaisha wananchi 28,671, anaripoti ALLAWI KABOYO.
Akizungumza katika hafla ya kuufunga mradi huo iliyofanyika Agosti 26, mwaka huu na kuhudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukoba, Kadole Kilugala aliyemwakilisha mkuu wa wilaya hiyo pamoja na baadhi ya wananchi wanufaika wa mradi, Mkurugenzi wa Miradi Shirika la World Vision Tanzania, John Masenza alisema,mradi wa Kata Katerero umeweza kuhudumia vijiji 10 na kata nne ambapo umenufaisha watu 39,090 huku wanufaika wa moja kwa moja wakiwa 28,671.
Masenza alisema,wanufaika wameweza kujifunza shughuli za kilimo, ufugaji ,ujasiriamali, uboreshaji wa afya maji na elimu na kugharimu shilingi bilioni 12.7 kwa muda wa miaka 17 ya mradi huo.
Hata hivyo, alisema kuonekana kwa mafanikio hayo ni kwa ushirikiano wa Serikali na shirika kwa ufadhili wa nchi ya Australia iliyokuwa ikitoa pesa ya huduma hizo.
Katibu Tawala wa Wilaya Bukoba, Kadole Kilugala alisema,ujuzi uliojengwa kwa wananchi wa kata nne ndani ya wilaya hiyo utasaidia kuwafaa kipindi chote ambacho shirika halitakuwepo.
"Tambueni mtu anayekupa ujuzi wa jambo la kujitegemea ni mzuri kuliko yule anayekupa leo, halafu kesho usimuone tena, niwaambieni ujuzi huu utumieni nyakati zote shirika linapokuwa halipo,"alisema Kilugala.
Vile vile Kilugala alisema, mashirika yanayoleta ufadhili kwa jamii yanasaidia kuongeza msukumo wa maendeleo kwani yanaweka mchango wake kwa Serikali kusaidia jamii ambayo inauhitaji muhimu.,
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wa Kata ya Katerero Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wameiomba Serikali kuwapatia ufahamu wa jinsi ya kuendesha miradi ya maendeleo kwa jamii inayoanzishwa na Serikali pamoja na wafadhili mbalimbali ili kuleta matokeo chanya yatokanayo na miradi hiyo.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Katerero wakitoa
burudani kwenye hafla ya kufunga mradi wa Katerero AP unaofadhiliwa na Shirika
la World Vision Tanzania. Picha na ALLAWI KABOYO/www.diramakini.co.tz |
Johanes Joel mkazi wa Kata ya Katerero alisema, miradi inayoletwa inawalenga wananchi kuwabadilisha kwenye maisha na kupiga hatua ya maendeleo kwa kile kinachokusudiwa.
"Bila kupewa kwanza ufahamu inakuwa vigumu kuyafanya na kuonyesha mwitikio kwani hatuna mwanga wa kuendesha wenyewe na kupata kitu chanya,"alisema Joel.Kata Bujugo alisema kuwa, wingi wa miradi inategemewa wananchi kupewa elimu ya kufahamu jambo na kutoka kwenye utegemezi wa ndugu na Serikali.
Aidha, alisema idadi kubwa ya mashirika yanatoa elimu wezeshi kwa jamii kabla ya kuwapatia mradi na hukakikisha kundi linasimama lenyewe na kunufaika kama wanavyotegemea.
"Jamii inamwitikio endapo itatambua kile kinacholetwa kinahitaji nini kwa jami na kufundisha na kufikia wengine kutoka kwenye umasikini mimi nayapongeza mashirika,"alisema Hamlungi.
Mratibu wa Mradi wa Katerero AP, Atugonza Kyaruzi
akitoa ufafanuzi wa namna wananchi walivyonufaika na mradi wa Katerero AP kwa
wananchi na mgeni rasmi.Picha na ALLAWI KABOYO/www.diramakini.co.tz |
Sharifa Kakulwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii Kata Katerero alisema, kupitia Shirika la World Vision wananchi wameweza kuunda vikundi zaidi ya 300 ambavyo vinanufaika na uchumi, kilimo,afya, elimu na maji.
Aliongeza kuwa,kundi la wanawake limeamka na kujiamini kuanzisha uzalishaji ambao unawapatia kipato na kuendesha maisha yao tofauti na hapo awali.