World Vision Tanzania yaisaidia Serikali kuboresha miradi ya kijamii

 SHIRIKA lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania limekabidhi jengo la wodi ya mama na mtoto ikiwa ni moja ya ahadi walioitoa katika Kituo cha Afya Rubale, baada ya kuwepo kwa changamoto hiyo kwa akina mama wajawazito kwa kipindi kirefu, anaripoti Allawi Kaboyo kutoka Bukoba.

Mgeni rasmi Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Msela Bumbuli (kulia) akikatata utepe n George Leo (kushoto) kuashiria kukamilika kwa makabidhiano ya jengo la mama na mtoto lililojengea na Shirika la World Vision Mradi wa Rukoma A P Kituo cha Afya Rubale. Picha na Allawi Kaboyo/Diramakini.

Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika katika Kituo cha Afya Rubale kilichopo Halmashauri ya Wilaya Bukoba mkoani Kagera na kuhudhuriwa na baadhi ya wananchi wanaotumia kituo hicho pamoja na uongozi wa Kijiji cha Rubale.

Akizungumza kabla ya kukabidhi jengo hilo kwa niaba ya Meneja wa shirika hilo Kanda ya Kagera, George Leo amesema kuwa, shirika hilo limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali hapa nchini na kwa upande wa Mradi wa Rukoma AP wamejenga vyumba vya madarasa katika shule  mbalimbali, wametengeneza madawati, wamejenga vyoo, nyumba ya mwalimu na wodi ya mama na mtoto.

 

Mratibu wa Mradi wa Rukoma A P, Lugembe Ng’oga akitoa maelezo kwa mgeni rasmi pamoja na wananchi juu ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto  Kituo cha Afya Rubale kwa ndani na matumizi yake. Picha na Allawi Kaboyo/Diramakini.

 

Leo amesema kuwa, Mradi wa Rukoma A P ulianza kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 ambapo mpaka mwaka huu wanajivunia kufanikisha baadhi ya miradi walioitekeleza huku mradi wa wodi ya mama na mtoto Kituo cha Afya Rubale hadi kukamilika kwake imetumia kiasi cha shilingi milioni 118 fedha za kitanzania.

“Shirika letu linalenga sana kumuhudumia mtoto, na sisi katika kuhakikisha mtoto anakuwa salama tanajitahidi kuboresha miundombinu kama kuboresha upande wa kumpatia elimu mtoto iliyo bora, afya ya mtoto, lishe na maji safi na salama. Kituo hiki kilikuwa zahanati na baadae kupandishwa hadhi ya kuwa kituo cha afya hali hiyo ilipelekea watoto na watu wazima kulazwa katika wodi moja na hilo ndilo lililotupelekea sisi kuomba ufadhili wa kujenga wodi hii,"amesema.

 

George Leo aliyesimama akitoa taarifa ya Mradi wa Rukoma A P kwa mgeni rasmi na wananchi waliohudhuria kwenye hafla ya makabidhiano ya wodi ya mama na mtoto Kituo cha afya Rubale kwa niaba ya Meneja wa Shirika la World Vision Kanda ya Kagera. Picha na Allawi Kaboyo/Diramakini.

Ameongeza kuwa, jengo hilo tayari limekamilika ambapo ameiomba Serikali kuhakikisha inamalizia masuala ya upatikanaji wa maji, vifaa tiba, wahudumu na kuliwashia umeme ili lianze kutumika kwa wananchi, kwa lengo lililokusudiwa huku akiwaomba wananchi kulitunza jengo hilo.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba,Msela Bumbuli akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, amelishukuru Shirika la World Vision kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwajali wanyonge kwa kuwaboreshea maisha.

Wananchi pamoja na wahudumu wa kituo cha afya wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi, Msela Bumbuli (wa tatu) kutoka kushoto pamoja na watumishi wa Shirika la World Vision baada ya makabidhiano ya jengo la wodi ya mama na mtoto Kituo cha Afya Rubale. Picha na Allawi Kaboyo/Diramakini.

Amesema kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo kwenye jamii itasaidia kuinua uchumi kwa kuwa maisha sasa yatakuwa rahisi, kwa upande wa afya watakuwa wanapata huduma bora na sahihi na kuongeza kuwa jengo lililojengwa linakidhi mahitaji na kuahidi kulitunza kwa maslahi ya wananchi.

Aidha, Bumbuli amesema kuwa, changamoto zilizobakia Serikali itahakikisha inazimaliza kama maji umeme, vifaa tiba na wahudumu wa afya ambalo hilo amesema ni jukumu la Serikali ili kuhakikisha malengo ya jengo hilo yanatimia huku akizidi kuliomba shirika kuendelea kuisaidia Serikali.

Muonekano wa jengo la wodi ya mama na mtoto Kituo cha afya Rubale lililojengwa na Shirika la World Vision Tanzania kupitia Mradi wa Rukoma A P likiwa limegharimu kiasi cha shilingi milioni 118 fedha za kitanzania hadi kukamilika kwake. Picha na Allawi Kaboyo/ Diramakini.

Creophas Bugingo ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Rubale ameshukuru shirika kwa kuwapatia jengo hilo ambalo litatoa fursa kwa wanawake wajawazito kujifungua kwa usalama huku mganga mfawidhi wa kituo hicho, Daktari Tuvatus Madio amesema kuwa, ujio wa kituo hicho utasaidia utoaji wa huduma kuboreka na kitasaidia wodi iliyokuwa ikitumika kama wodi ya wanawake itatumika kwa ajili ya wanaume maana hapo awali wodi ya wanaume haikuwepo.

Baadhi ya akina mama waliohudhuria hafla hiyo wakizungumza kwa furaha ya kupata jengo hilo wameeleza adha walizokuwa wakizipata hapo awali kuwa walikuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kwenda Hospitali Teule ya Izimbya ili kujifungua kwa usalama.

Wamesema kuwa, walikuwa wakidhalilika sana kwa kukosa jengo la mama na mtoto na wengine kupelekea kujifungulia barabarani kwa kukosa msaada wa haraka na stara ya kibinadamu.

Kituo cha Afya Rubale nje ya kutokuwa na wodi maalumu ya wanaume kina changamoto ya chanzo sahihi cha maji cha kudumu maaana hutegemea maji ya mvua, hali inayowapelekea wanaopata huduma kituoni hapo kuathirika pamoja na jiko kwa ajili ya wanaowahudumia wagonjwa ikiwemo upungufu wa watumishi huku waliopo wakiwa 13.

 

Je, una habari,maulizo au tangazo? Tuwasiliane; diramakini@gmail.com

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news