BALOZI KIJAZI AWATAKA WAHANDISI KUTUMIA TEKNOLOJIA KUONGEZA KASI YA MAENDELEO

SERIKALI imewataka wahandisi kutumia fursa za kiteknolojia kuleta maendeleo chanya katika uzalishaji na ukuzaji wa uchumi wa viwanda nchini.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi akifungua mkutano wa 17 wa Siku ya Wahandisi uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma leo.

Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 17 wa Wahandisi jijini Dodoma, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi, ameshauri wahandisi kuzingatia maeneo matatu muhimu ili kuleta mabadiliko chanya kwa wakati.

Sehemu ya wahandisi 400 wakila kiapo cha utii katika Mkutano wa 17 wa Wahandisi uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Viongozi mbalimbali wa Serikali wakitambulishwa kwenye Mkutano wa 17 wa wahandisi uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Ameyataja meneo hayo kuwa ni kufanya mabadiliko kwenye utoaji wa elimu ya uhandisi kwenye vyuo vya kufundishia na kwenye mafunzo kazini, kuwekeza zana na vifaa vipya ambavyo vinavyoendana na mapinduzi ya nne ya viwanda na kubadili utamaduni wa kazi katika sekta ya uhandisi ambapo itafanya wahandisi waongeze uhusiano na fani nyingine.

“Mkizingatia maeneo haya ambayo yanaonekana kuwa changamoto kwenu na kuyabadili kuwa fursa, itasaidia katika kuleta mabadiliko katika ulimwengu huu wa mapinduzi ya nne ya viwanda,"amesisitiza Balozi Kijazi.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi, akimkabidhi tuzo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Nicholas Mkapa, ikiwa ni kuenzi mchango wa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa, katika kuwezesha ukuaji wa sekta ya uhandisi nchini.

Ameongeza kuwa, kwa wahandisi ambao wanauelewa wa mabadiliko ya mapinduzi ya nne ya viwanda wanaweza kutoa elimu kwa wahandisi wengine ili kuongeza ujuzi kwa ujumla.

Aidha, amewataka wahandisi hao kupitia mkutano huo kuja na mapendekezo ya kisera na kisheria ya aina ya maendeleo ambayo yataifanya nchi iwe tayari kupitia wahandisi wake kushiriki maendeleo ya mapinduzi ya nne ya viwanda kwa viwango vya kimataifa.

Amesisitiza umuhimu wa wahandisi kuwa tayari na kuhakikisha wanajijengea uwezo unaohitajika ili kuweza kutumia fursa hizo kikamilifu na kufanya kazi zao kwa weledi na uadilifu mkubwa.

“Jitahidini kukamilisha miradi yote vizuri kwa muda uliopangwa na kwa thamani iliyo halisi ili kukuza uchumi,”amesema Balozi Kijazi.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, mara baada ya kukagua maonesho ya shughuli za kihandisi katika maadhimisho ya  17 yaliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch.Elius Mwakalinga, amesema kuwa lengo la Serikali ni kuwa na wahandisi 80,000 hadi kufikia mwaka 2025.

“Idadi hii itawezesha utekelezaji wa malengo 17 ya dunia (SDGs), kwa wakati ambayo yanagusa ukuaji wa huduma za viwanda, afya, maji, umeme, miji endelevu na jamii yenye usawa wa kijinsia, kazi nzuri na ukuaji wa uchumi,”amebainisha Arch. Mwakalinga.
Msajili wa Bodi ya Wahandisi, Mhandisi Patrick Barozi akitoa taarifa ya utendaji wa bodi hiyo katika Mkutano wa 17 wa Wahandisi uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Profesa Ninatubu Lema, amesema hadi sasa jumla ya wahandisi 3761 kati ya 6552 wameshakula viapo vya utii na wahandisi 452 wameapa katika maadhimisho hayo ya 17.

Mkutano huu wa 17 wa wahandisi wenye kauli mbiu ya Mapinduzi ya nne ya viwanda ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu: changamoto na fursa kwa wahandisi, umefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na zaidi ya wahandisi 2,500 wa fani mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na zaidi ya wahandisi 3,500 wamefuatilia mkutano huo kwa njia ya mtandao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news