Wakili Fatma Karume aondolewa katika orodha ya Mawakili Tanganyika

Kikao cha Kamati ya Maadili ya Mawakili kilichokaa leo Septemba 23,2020 kimemkuta na hatia ya kukiuka maadili kwa kiwango cha juu, Wakili Fatma Karume mwenye roll namba 848 na hivyo kuamuru jina lake liondolewe (permanent removal) katika orodha ya Mawakili Tanganyika, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Septemba mwaka 2019, Wakili Karume maarufu kama Shangazi alisimamishwa kufanya kazi ya Uwakili Tanzania Bara, maamuzi yaliyotolewa na Jaji Feleshi kwenye kesi iliyofunguliwa na Ado Shaibu akipinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuteuliwa kimakosa na Rais Dkt.John Magufuli na kesi iliondolewa.

Mahakama Kuu iliamuru Fatma Karume apelekwe Kamati ya Maaadili ya Mawakili kwa kosa la kushambulia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambae ndiye alikuwa Wakili wa Ado Shaibu katika kesi hiyo.

Akijibu hoja ya mdau kwenye mtandao wa Twitter aliyemuomba akate rufaa dhidi ya uamuzi huo, Fatma Karume amesema hatafanya hivyo kwa maelezo kwamba muamuzi wa rufaa yake sio huru.

"Ukiingia kwenye mapambano unahitaji kujua nani unapambana nae, kanuni za mpambano na uhuru wa muamuzi. Iwapo kanuni haziko wazi na muamuzi hayuko huru, huo sio mpambano bali upotevu wa muda. Hifadhi nguvu zako kwa mpambano unaoweza kushinda,"majibu ya Shangazi.

Fatma Karume ni nani?

Fatma Karume ambaye alizaliwa 15 Juni 1969 ni mwanasheria wa Kitanzania na wakili wa kujitegemea, mwanaharakati ambaye aliwahi kuwa Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2019.

Alipata wadhifa huo baada ya kushinda katika uchaguzi wa urais wa chama hicho uliofanyika Aprili 2018 na hivyo kumrithi mtangulizi wake Tundu Lissu aliyekiongoza chama hicho kutoka mwaka 2017 hadi 2018.

Fatma ni mtoto mkubwa wa Rais wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani Abeid Karume na ndugu zake wengine ni Abeid, Shuwana na Ahmed.

Ni mjukuu wa Rais wa Awamu ya Kwanza wa Zanzbar, Sheikh Abeid Aman Karume.

Kwa upande wa elimu yake ya masuala ya kisheria kwa kiasi kikubwa amesomea nchini Uingereza.Amefanya kazi kwa muda mrefu katika Kampuni ya IMMA Advocates ya jijini Dar es Salaam katika kusimamia masuala ya mashitaka mahakamani kabla ya uamuzi tajwa juu kufanyika.Yaliyomkuta kazini Fatma Karume soma hapa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news