BREAKING NEWS: Waganga wa kienyeji jela kwa rushwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Babati mkoani Manyara imewahukumu Luhanga Mindi Mabeshi na Hamisi Juma Gambona kwenda kutumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kuwakuta na hatia ya kuomba rushwa ya sh.500, 000 na kupokea sh.200, 000 kinyume cha kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na 11/2007.
Hukumu hiyo ilitolewa tarehe 9 Septemba 2020 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Babati, Simoni Kebello katika Shauri Na. CC.05/2019 baada ya kusikiliza pande zote mbili na kuridhika na ushahidi uliowasilishwa bila kuacha shaka yoyote na upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na wakili wa TAKUKURU, Eveline Onditi.

Awali washtakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo kwa makosa ya kudai na kupokea rushwa kutoka kwa Mganga wa Jadi - Wilayani Babati. Washtakiwa walifika wilayani Babati na kujitambulisha kama wapelelezi kutoka Umoja wa Waganga wa Jadi na Tiba Asili Tanzania (UWAWATA).

Kwamba kwa cheo hicho walikwenda kumkagua mmoja wa waganga wa jadi kisha kumtuhumu kuwa wamemkuta akifanya shughuli za uganga kwa kutumia ramli chonganishi kinyume na taratibu za uganga hivyo wakamtaka mganga huyo wa jadi atoe rushwa ili wasimchukulie hatua.  

Mganga huyo wa jadi kwa kuwa hakuwa anafanya ramli chonganishi kama ilivyodaiwa, aliamua kutoa taarifa TAKUKURU iliyopelekea kukamatwa kwa Mabeshi na Gambona wakiwa wamepokea shilingi laki mbili (sh.200,000) na kisha kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa.

Wakati hukumu hii ikitolewa mshtakiwa Luhanga Mabeshi hakuweko mahakamani kwa kuruka dhamana, hivyo mshtakiwa wa pili Hamis Gambona amepelekwa gerezani kuanza kutumikia kifungo,

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Makungu ameongeza kuwa, “ni rai yetu kwa raia wema popote watakapomuona Luhanga Mindi Mabeshi watoe taarifa ofisi ya TAKUKURU iliyo karibu ili aweze kukamatwa na kupelekwa kutumikia adhabu yake. Mabeshi hupenda kutembelea maeneo ya Karatu Mkoani Arusha na mkoani Shinyanga,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news