Membe ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliidhinishwa na chama kwa kura za ndio 410 sawa na asilimia 97.61 ya kura zilizopigwa, huku kura za hapana zikiwa 10 sawa na asilimia 2.39 za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Uanachama wa Bernad Membe ndani ya ACT- Wazalendo ulitangazwa mwezi Julai, mwaka huu na Kiongozi Mkuu wa chama, Zitto Kabwe katika mkutano wa wanahabari, wadau wengine kutoka sehemu mbalimbali Duniani ambao ulifanyika kwa njia ya mtandao.
Diramakini imejiridhisha kuwa, kulingana na miongozo ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa huenda, uamuzi wa Maalim Seif kuutangazia umma kuwa, wanamuidhinisha Tundu Lissu kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku yeye akiwania Urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, hivyo kutumia nafasi hiyo kumnadi Lissu ulikuwa batili.
Mgombea wa Urais huyo wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha ACT
Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad alimnadi mgombea wa Urais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrsia na Maendeleo
(CHADEMA), Tundu Lissu katika mkutano wake wa kampeni na kueleza kuwa
ana imani atakuwa Rais wa Tanzania.
Maalim Seif aliyaeleza hayo katika Uwanja wa Mpira wa Mwanakombo katika Jimbo la Mohonda Wilaya ya Kaskazini B Unguja katika mfululuzo wa kampeni zake visiwani humo.
Amesema, hana wasiwasi kuwa, Lissu atakuwa Rais na amesema akiingia
madarakani mgombea huyo wa CHADEMA na yeye akiwa Rais wa Zanzibar siku
ya pili tu baada ya kuapishwa atamtaka amkabidhi Mashekhe wa Zanzibar
ambao wamewekwa ndani Tanzania Bara.
“Imani yangu Lissu atakuwa
Rais wa Tanzania na mimi nitakuwa wa Zanzibar itakuwa raihisi Mashekhe
wetu kuwarejesha.Lakini ikitokea bahati mbaya akirudi huyo Magufuli na mimi nikiwa Rais nitamtumia ndege, lazima awatowe watu wangu,”amesema.
Kupitia barua iliyoonwa na Diramakini kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, imejiridhisha kuwa, Bernard Membe bado ni mgombea halali wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ACT- Wazalendo, hivyo aliyoyasema Maalim Seif hayakuwa na visaidizi vyovyote vya kuuthibitishia umma kuwa,utambuzi huo utakuwa endelevu baina ya ACT-Wazalendo na CHADEMA.Unaweza kuisoma barua hapa chini.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imesisitiza kuwa, vyama vya kisiasa vinapaswa kuheshimu sheria vinapoingia katika ushirikiano wa aina yoyote ama miungano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, Msajili amesema kwamba, vyama hivyo vinapaswa kuwasilisha ushirikiano au muungano huo kwake miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.
Membe agomea
"Mimi ndiyo Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT- Wazalendo. Mimi ndiye niliyekabidhiwa Ilani ya chama hicho kuinadi kote nchini kwenye uchaguzi huu. Taarifa zinazosambaa kuwa tayari tumejiunga na Chadema katika ngazi ya Urais siyo za kweli".
Mchambuzi wa masuala mbalimbali wa Diramakini amebainisha kuwa, kwa hatua hiyo, Bernard Membe hawezi kutatizwa na jambo lolote, labda atimuliwe uanachama ACT-Wazalendo, ndiyo maana huenda Kiongozi Mkuu, Zitto Kabwe ameueleza umma kuwa, wavute subira hadi Oktoba 3, mwaka huu ili waweze kupata jawabu kamili ya nini kinachoendelea.
Septemba 22, mwaka huu Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo , Zitto Kabwe amesema vyama vya upinzani nchini vimekubaliana kumuunga mkono Mgombea mmoja wa Urais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania na pia, kwa upande wa Zanzibar.
Zitto ameongeza kuwa Oktoba 3, 2020 watatangaza ni nani hasa atasimama
kama Mgombea Urais katika mkutano wa hadhara utakaohusisa CHADEMA, ACT
Wazalendo na vyama vingine vya upinzani.
Amesema ACT-Wazalendo
wameshajadiliana na wameshawasilisha mapendekezo yao kwa CHADEMA na
baada ya pande zote kukamilisha mazungumzo watatangaza makubaliano
yatakayofikiwa.