BREKING NEWS: TAKUKURU YAMNASA MWALIMU AKITAKA KUMHONGA KATIBU TAWALA

 

 
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tabora inategemea kumfikisha mahakamani mwalimu kwa tuhuma za kutoa rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1) (b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo amesema kupitia taarifa iliyoonwa na www.diramakini.co.tz kuwa, KONDWANI PETER MASATA ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Kizengi Kata ya Kizengi Wilaya ya Uyui Mkoa wa Tabora,leo Septemba 7,2020 atafikishwa mahakamani kwa kosa la kutoa rushwa ya shilingi 90,000 kama kishawishi kwa Katibu Tawala Mkoa wa Tabora ili aweze kuhamishiwa Manispaa ya Tabora.

"Uchunguzi wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora uliofanyika umebaini kuwa mtuhumiwa aliomba uhamisho na kwa nyakati tofauti amekuwa akishawishi kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (SMS) na baadae kutoa fedha kiasi cha shilingi 90,000 kwa njia ya simu kama kishawishi ili aweze kuhamishiwa Manispaa ya Tabora toka Kizengi.
 
"Katika hatua nyingine TAKUKURU Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka leo tarehe 7 Septemba, 2020 inataraja kuwafikisha Mahakamani FIDELIS GABRIEL MYOVELLA Mhasibu wa Chuo va Ualimu Tabora na JOSEPH ROBERT KAIZEREGE Mfanyabiasha katika Manispaa ya Tabora kwa kosa la kutumia nyaraka kumdaganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya Mwaka 2007 ikisomwa pamoja na Aya ya 21 Jedwali la Kwanza na kifungu cha 57((1) na 60(2) ya Sheria ya Uhujumu Uchumi (Sura 200 Marejeo ya mwaka 2002)

"Inadaiwa kwamba, Fideli Gabriel Myovella akiwa mwajiriwa wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Chuo cha Ualimu Tabora alitumia nyaraka ya kuombea vifaa yenye maelezo ya uongo kuonyesha kuwa kampuni ya KANIJA & SONS ENTERPRISES wana haki ya kulipwa shilingi 12,214,000 kama malipo ya kusambaza vifaa vya umeme kwa ajili ya ukarabati wa Chuo cha Ualimu Tabora wakati akijua kuwa sio kweli.

"Vilevile Joseph Robert Kaizerege kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake - Mkuu wa Chuo Chuo cha Ualimu Tabora alitoa hati ya madai yenye  maelezo ya uongo kuonyesha kuwa Kampuni ya KANIJA & SONS ENTERPRISES wanadai kiasi cha shilingi milioni 12,214,000 kama malipo ya vifaa vya umeme kwa ajili ya ukarabati wa Chuo cha Ualimu Tabora.

"Ninawashukuru wananchi wa mkoa wa Tabora kwa ushirikiano mnaoutoa kwa TAKUKURU na ninawaasa watumishi na wananchi wa mkoa wa Tabora kutojihusisha na vitendo vya rushwa. TAKUKURU tutahakikisha kuwa tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote wasio waadilifu.

"Aidha, kama mnavyofahamu, Taifa letu lipo katika harakati za uchaguzi ambapo wagombea wameanza kupita pita na kunadi sera zao. Tafadhali tuwasikilize kwa makini na tusiwakubali wagombea wanaoturubuni kwa rushwa.  Tutoe taarifa ya vitendo vya rushwa kupitia TAKUKURU APP au namba 113 (Bure) au fika ofisi za TAKUKURU zilizopo wilaya zote za Mkoa wa Tabora,"ameeleza Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo kupitia taarifa iliyoonwa na www.diramakini.co.tz

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news