Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara nchini (BRELA) idara ya usajili wa makampuni na majina ya biashara, Meinrad Rweyemamu amesema kuwa, wakala huo unafanya kazi ya kufungua milango kwa wafanyabiashara ili waweze kuendesha kazi zao bila vikwazo vya kibiashara,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini),Geita.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usajili wa Makampuni na Majina ya Biashara kutoka BRELA, Meinrad Rweyemamu akizungumzia malengo ya wakala huo kushiriki maonyesho ya teknolojia ya madini mjini Geita. (Diramakini).Amesema hayo katika maonyesho ya tatu ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika kijiji maalum cha maonyesho mjini Geita ambapo BRELA wanashiriki maonyesho hayo.
Rweyemamu ameongeza kuwa, BRELA wanafanya kazi mbalimbali ikiwemo kusajili makampuni, majina ya biashara na kusajili ubunifu kwa mtu aliyevumbua kitu kipya.
Kazi nyingine amesema kuwa, ni kusajili alama za biashara,kutoa ushauri kwa wafanyabiashara wanaotaka kufanya kazi zao za kibiashara na kutoa ushauri jinsi ya kumaliza migogoro inapokuwa imetokea katika biashara zao.
Rweyemamu ametaja kazi nyingine za BRELA ni kutoa leseni za daraja la kwanza kwa ajili ya biashara kubwa na leseni za viwanda mbalimbali.
Pia amewaomba wafanyabiashara kanda ya ziwa kutumia maonyesho hayo kufika katika banda la BRELA ili kurasmisha biashara zao kwa kusajili majina ya biashara na makampuni ili waweze kufanya biashara zao bila matatizo.
Afisa wa BRELA, Christina Njovu akitoa maelezo kwa mteja aliyefika katika banda la wakala huo katika maonyesho ya teknolojia ya madini mjini Geita kwa ajili ya kupata huduma. (Diramakini).
Ametaja faida za kusajili majina ya biashara na Makampuni kuwa ni pamoja kuaminika kwa wadau wengine wa kibiashara kama taasisi za kifedha kama vile benki na washirika wengine.
Rweyemamu amesema kuwa, kwa sasa BRELA inafanya usajili kwa njia ya mtandao wa intaneti na mteja anatakiwa kuwa na kitambulisho cha taifa kinachotolewa na Mamlaka ya NIDA pamoja na ada ya usajili.
Amewaomba wachimbaji ambao wanafanyabiashara ya madini kusajili majina ya biashara na makampuni au kusajili vifaa ambavyo wamevigundua vinavyotumika kuchimba madini yao.
BRELA inaendelea kutoa huduma kwa wafanyabiashara katika maonyesho ya teknolojia ya madini mjini Geita kwa siku kumi mfululizo ili kuhakikisha inawafikia wafanyabiashara wengi katika Ukanda wa Ziwa.