MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Njombe, Rose Mayemba ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa, Oktoba 28, mwaka huu wanachagua viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais ili washirikiane nao kuharakisha maendeleo ikiwemo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakalibi.
Mayemba ametoa rai hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea wa ubunge Jimbo la Makambako,ambapo amewataka wanachama na wananchi kwa ujumla kuhakikisha hawafanyi makosa katika Uchaguzi Mkuu.
Amesema,CHADEMA wamejipanga kushinda katika
uchaguzi huo kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais katika maeneo yote
ambayo wamesimamisha wagombea nchini.“Tuleteeni mtu ambaye akienda kupaza sauti kule huku utakuta maji
yanatanda,na mchagueni General Reuben Kaduma kwa sababu ana ajenda za Makambako
na ajenda za kitaifa,"amesema Mayemba.
Kwa upande wake mgombea wa ubunge Jimbo la Makambako, General Reuben Kaduma amesema
endapo atapata ridhaa kwa wananchi na kuwa mbunge atahakikisha
anawasaidia wananchi katika kutatua changamoto zinazowakabili katika
sekta ya kilimo,afya,maji na elimu.
“Dhamira ni kuwaletea heshima na maendeleo Makambako,watu wanahusika
kwenye biashara,kilimo lakini manufaa ni madogo,nimeona niweze
kuwatumikia Wanamakambako ili tuweze kusonga mbele,”amesema Kaduma.
Aidha, baadhi ya wagombea wa udiwani kupitia chama hicho akiwemo
mgombea udiwani Kata ya Makambako, Daud Tweve,mgombea udiwani Kata ya Kivavi, Baraka ivambe,mgombea udiwani Kata ya Mwembetogwa, Sillas Makweta na mgombea udiwani Kata ya Kitisi, Seth Vegulla wamewaomba wananchi kuwapatia kura zao kwa kuwa wana ajenda za kimaendeleo katika kata hizo ambazo zinalenga kuwakomboa kiuchumi.
Katika hatua nyingine, mgombea Urais kupitia CHADEMA,Tundu Lissu katika kampeni zake zilizofanyika mkoani Morogoro leo Septemba 11,2020, amevitaja vipaumbele vyake ambavyo ni haki , usawa na maendeleo ya watu.
Lissu katika kampeni hizo amewataka wananchi hao kufanya maamuzi sahihi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu ili kupata Rais mwenye kujali uhuru na kuleta maendeleo.
"Niwaombe wana Morogoro muwachague viongozi waliobaki na ambao watarudishwa kwenye rufaa muwapigie kura ili mpate maendeleo,"amesema huku akifanya harambee ya kuchangia kampeni hizo, ambapo amedai kuwa ili kampeni ziendelee lazima wasaidiane, "...pia nimepigwa kiuchumi, nilikua Mbunge na mnajua ulipoishia sasa hii kampeni tunaimalizaje inabidi tusaidiane, mimi nawaombeni mtuchangie sioni aibu,"amesema.